Mwambusi, Pluijm, Goran vitani kocha bora VPL 2014/15



Mwambusi, Pluijm, Goran vitani kocha bora VPL 2014/15

IMG_9807

Juma Mwambusi (kushoto)

"Mwambusi alitwaa tuzo ya kocha bora wa VPL msimu wa 2013/14 ambao ulikuwa wa kwanza kwa timu yake ya Mbeya City Ligi Kuu."

MSIMU wa 2014/15 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ulimalizika juzi huku Ruvu Shooting Stars na Police Morogoro zikiporomoka daraja.

Tayari winga hatari wa Yanga aliyekulia Azam FC, Simon Msuva, ameshajihakikishia tuzo ya kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa msimu akifunga mabao 17 ikiwa ni sawa na idadi ya mabao ambayo mfungaji bora wa VPL msimu wa 2012/13, Kipre Tchetche wa Azam FC alifunga.

Bado haijajulikana wanasoka watakaokabidhiwa tuzo ya kocha bora, kipa bora, mchezaji bora na refa bora wa VPL 2014/15, lakini katika kipengele cha kocha bora vita inaonekana wazi kuwahusisha Mdachi Hans van der Pluijm wa Yanga, Mserbia Goran Kopunovic wa Simba, Mganda Jackson Mayanja wa Kagera Sugar na wazawa Juma Mwambusi wa Mbeya City na Felix Minziro wa JKT Ruvu na Mecky Mexime wa Mtibwa Sugar.

JUMA MWAMBUSI – MBEYA CITY

Kocha bora wa VPL msimu wa 2013/14, Juma Mwambusi, ana nafasi kubwa ya kuitwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo endapo vigezo vya msimu huo vitatumika kwa mara nyingine kumpata kocha bora wa ligi hiyo msimu uliomalizika juzi.

Wakati wa kukabidhi zawadi za VPL msimu wa 2013/14, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilieleza kuwa miongoni mwa sifa za kocha bora wa msimu ni kuiongoza timu katika mechi zote za msimu. 

Mwambusi na makocha wengine sita; Mayanja, Mexime, Minziro, Bakari Shime wa Mgambo Shooting na Tom Olaba wa Ruvu Shooting waliofanikiwa kuumaliza msimu huu bila kufukuzwa. Mwambusi aliandika barua ya kuacha kazi ya kuinoa City Novemba mwaka jana, lakini uongozi wa timu hiyo ulikataa ombi lake.

Licha ya kuanza vibaya msimu kwa kupoteza mechi nne mfululizo kuanzia raundi ya nne hadi ya saba, Mwambusi ameiwezesha Mbeya City kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa VPL ikikusanya pointi 34 baada ya kushinda mechi nane, sare 10 na kupoteza mechi nane. City ilimaliza nafasi ya tatu katika msimu wake wa kwanza VPL wakati Mwambusi akiibuka kocha bora.

 

HANS VAN DER PLUIJM – YANGA

Pluijm ameiongoza Yanga katika mechi 19 za VPL akishinda mechi 13, sare tatu na kupoteza tatu pia. Alitua Desemba mwaka jana kurithi mikoba ya Mbrazil Marcio Maximo, aliyetimuliwa baada ya kushinda mechi nne za VPL sare moja na vipigo viwili.

Kutokana na kuipa taji Yanga, tena ikiwa na mechi mbili mkononi, Pluijm ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya kocha bora wa msimu, lakini kigezo cha kuingoza timu katika mechi zote 26 kitamwangusha endapo TPLB itakitumia tena kumpata mshindi.

GORAN KOPUNOVIC – SIMBA

Mserbia huyu ameiongoza Simba katika mechi 18 za VPL akiisaidia kumaliza nafasi ya tatu, moja zaidi ya ilivyokuwa msimu wa 2013/14.

Kopunovic, aliyesaini mkataba wa miezi sita siku ya Mwaka Mpya, aliikuta Simba ikiwa nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi ikiwa imeshinda mechi moja, sare sita na kupoteza moja. Katika mechi zote 18 za ligi, kocha huyo amekusanya pointi 38 akishinda mechi 12, sare mbili na kupoteza mechi nne.

Mbali na kuwa timu pekee iliyozifunga Yanga na Azam FC msimu uliomalizika juzi, mafanikio ya Simba na ubora wa soka ulioonyeshwa na timu hiyo ya Msimbazi ikiwa imefunga mabao 31 katika mechi 18 chini ya Kopunovic, yanampa nafasi kocha huyo kutwaa tuzo ya kocha bora wa msimu, lakini kigezo cha kuingoza timu katika mechi zote 26 kitamwangusha endapo TPLB itakitumia tena kumpata mshindi.    

 

JACKSON MAYANJA

Mganda huyu ni miongoni mwa makocha wachache ambao hawajatimuliwa na timu zao katika misimu miwili mfululizo iliyopita ya VPL. Msimu uliomalizika juzi Mayanja amefanikiwa kuna pointi 32 katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa VPL wakishinda mechi nane, sare nane na vipigo 10.

Hata hivyo, kukosekana benchini katika mechi mbili walizolala 2-1 dhidi Ndanda FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Januari 24 na sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Januari 31, huenda kukamnyima Mayanja nafasi ya kutwaa tuzo ya kocha bora wa msimu. 

Wakati mechi hizo zinachezwa, Mayanja alirejea kwao Ugand kuhudhuria kozi maalum ya Shirikisho la Soka barai Afrika kuhusu ukocha wa soka. 

Aidha, utovu wa nidhamu aliouonyesha kwa kutukana marefa na kuwatuhumu kuhongwa kulikosababisha apigwe faini na kufungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivi karibu, kunaonekana ni pigo kwa kocha huyo katika mbio za kocha bora wa VPL 2014/15.

MECKY MEXIME – MTIBWA

Mtibwa Sugar, mabingwa wa 1999 na 2000 wa Tanzania Bara, waliuanza vyema msimu kwa kuipiga Yanga 2-0 kisha kukaa kileleni kwa muda mrefu hadi Januari 24 walipofungwa 2-1 ugenini dhidi ya Ruvu Shooting.

Kutokana na kuyumba katikati mwa msimu, kikosi cha Mexime kimemaliza nafasi ya saba katika msimamo wa VPL kikiwa na pointi 31 baada ya kushinda mechi saba, kutoka sare mara 10 na kupoteza mechi tisa.

Kumaliza msimu bila kufukuzwa kunambeba nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars, Mexime, kutwaa tuzo ya kocha bora wa msimu endapo kigezo hicho kitazingatiwa tena TPLB kama ilivyokuwa msimu uliopita.

FELIX MINZIRO: JKT RUVU

'Maafande' wa JKT Ruvu waliuanza vibaya msimu kwa kutoka suluhu dhidi ya City kisha kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Kagera Sugar na Yanga.

Tangu ajiunge nao katikati ya msimu wa 2013/14 akitokea Yanga alikofukuzwa, Minziro amefanikiwa kuibadilisha JKT Ruvu Stars kutoka kucheza soka la butua butua hadi kusakata kandanda linalovutia na lenye pasi nyingi mithili ya Barcelona ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).

JKT Ruvu imemaliza nafasi ya nane katika msimamo wa VPL ikiwa na pointi 31 baada ya kushinda mechi nane, kutoka sare mara saba na kupoteza mechi 11.

Kudumu katika timu moja msimu mzima bila kufukuzwa, kunampa nafasi Minziro kuwania tuzo ya kocha bora wa msimu ingawa wapinzani wake, endapo kipengele cha kuongoza timu katika mechi zote 26 kikizingatiwa na TPLB, wamefanya vizuri zaidi. Makocha hao ni Mwambusi, Mayanga na Mexime.

Imeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi wa michezo mwandamizi wa gazeti la NIPASHE.

CHANZO: IPP MEDIA



Comments