KOCHA mkuu wa Simba, Goran Kopunovic bado hajafikia makubaliano na klabu yake kuhusu kusaini mkataba mpya, lakini tayari ameshawaambia wachezaji wake kuwa yupo katika mazungumzo na uongozi.
Kinachosababisha majaaliwa ya Kopunovic yasijulikane mpaka sasa ni dau kubwa analohitaji tofauti na bajeti ya Simba.
Ikumbukwe siku za karibuni uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Poppe ulikikiri kuwa klabu imeshuka kiuchumi kutokana na mashabiki kutokwenda uwanjani.
Baadhi ya wachezaji wa Simba wameeleza kuwa kama uongozi utashindwa kufikia makubaliano na kocha huyo basi watakuwa wamepoteza bonge la kocha.
"Kopunovic ni bonge la kocha, anajua kufundisha, ana msimamo, hababaishwi na viongozi kama ilivyokuwa kwa Phiri (Patrick) ambaye alikuwa anapangiwa wachezaji na mazoezi ya kuwapa wachezaji mechi ikikarabia." Amefafanua mchezaji wa Simba ambaye hakupenda jina lake kutajwa kwenye mtandao.
"Baada ya mechi ya mwisho na JKT Ruvu, kocha alikaa na sisi wachezaji, akatueleza kuwa wapo kwenye mazungumzo ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na akasema ikishindikana basi tutaonana panapo majaaliwa". Amesema mchezaji huyo na kuongeza: "Hata haya mambo ya kishirikina Kopunovic hapendi kabisa, ujue Simba kuna baadhi ya viongozi wanapenda sana mambo ya uchawi, eti hatuingii vyumbani na kutozwa faini, mara mganga anatwambia tuchelewe kuingia uwanjani, wachezaji wengine tuna imani zetu, yanatukera sana".
Wakati huo huo, imefahamika kuwa Simba inatarajiwa kutafuta makocha wengine kutoka nchi za Ufaransa, Bulgaria, Senegal na Serbia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe amekaririwa na Salehjembe akisema mipango ya kuleta kocha mpya ipo ikiwa watashindwana rasmi na Mserbia huyo na kuzitaja nchi hizo kuwa ndiyo zinazoweza kutoa kocha wao.
"Ikiwa tutashindwana na Kopunovic, kuna makocha kutoka nchi nyingi tu, wapo kutoka Ufaransa, Senegal, Bulgaria na hata Serbia huko ambapo anatokea yeye," alisema Hans Poppe alipohojiwa na SalehJembe.
Kuhusu usajili mpya ikiwa ni siku moja baada ya kutangaza wazi kutoendelea kuwa na beki Joseph Owino na Dan Sserunkuma kiongozi huyo alisema nako pia kuna wachezaji kutoka nchi kadhaa ambao wanajiandaa kuwaleta.
"Kuna wachezaji kutoka Ghana, Burundi, Kenya, Rwanda na Nigeria, kote huko tumeshapata maombi na mipango inafanyika kuja kufanya majaribio," alisema.
Comments
Post a Comment