KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij amesema timu yake ilifanya kila kinachowezekana kushinda dhidi ya Swaziland, lakini bahati haikuwa yao.
Katika mahojiano ya baada ya mchezo huo wa kwanza kwa Cosafa kwa Stars, Nooij aliwaambia SuperSport wanaorusha moja kwa moja michuano hiyo kuwa Taifa Stars ilishambulia zaidi na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini tatizo lilikuwa katika kupata bao.
"Tulicheza vizuri zaidi, tulipata nafasi zaidi lakini tulishindwa kupata bao la kusawazisha.
"Lengo lilikuwa angalau kusawazisha, lakini utaona hatukuweza kufanikiwa na utaona wenzetu wametumia nafasi moja tu waliyipata," alisema.
Stars imeanza michuano ya Cosafa kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Swaziland.
Baada ya kichapo hicho, Stars wanarudi kujiwinda na mchezo wa pili utakaopigwa mei 20 mwaka huu katika uwanja huo huo dhidi ya Madagascar majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika kusini, sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika mashariki.
Swaziland wao watachuana na Lesotho katika mechi ya pili ya kundi B.
Michuano ya Cosafa itaendelea leo kwa mechi mbili, Shelisheli watachuana na Zimbabwe majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika kusini sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Tanzania, baadaye majira ya saa 1:30 usiku kwa saa za 'Sauzi' sawa na saa 2:30 usiku kwa saa za Tanznaia, Namibia watakabiliana na Mauritius.
Comments
Post a Comment