Manuel Pellegrini amesema mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Wilfried Bony amemwangusha kwa kushindwa kutoa mchango alioutarajia katika kikosi cha Manchester City.
Wakati Pellegrini akimnunua Bony kutoka Swansea kwa dau la pauni milioni 28 katika usajili wa Januari, alikuwa na matumaini kwamba ataisaidia katika vita ya ubingwa wa Premier League na kuishinda Barcelona katika Champions League.
Lakini Bony alikosa mwezi wake wa kwanza tangu kusajiliwa kwa sababu ya majukumu katika kikosi cha Ivory Coast kwenye fainali za Mataifa ya Afrika, na tangu aliporudi amekuwa akiathiriwa na goti na kifundo cha mguu hali iliyomfanya kuanza katika mechi mbili tu na kufunga bao moja.
"Kwa kweli inakatisha tama. Tulimnunua kwa sababu tulikuwa na majeruhi katika washambuliaji," alisema Pellegrini na kuongeza kuwa hata hivyo ana uhakika staa huyo atashiriki vema mechi zilizobaki na kusaidia timu kupata nafasi ya Champions League msimu ujao.
Comments
Post a Comment