Mwanamuziki muimbaji na mtunzi mashuhuri wa bendi ya Maquis Original Mutombo Lufungula Audax, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, huko Kimara Michungwani. Mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa Mwananyamala Hospitali. Audax alikuwa ndie mmoja wa wanamuziki asili wa kundi la Maquis Du Zaire. Kundi la Maquis lilianza katika mji wa Kamina, jimbo la Shaba, huko Kongo. Awali kundi lilianza kwa kuitwa Super Teo, kisha kubadili jina na kuitwa Rocken Success na baadae Super Gabby na mwisho wakati wakiingia Tanzania mwaka 1972 walikuwa wakiitwa Maquis Du Zaire. Kundi hili la awali likuwa na wanamuziki tisa, na sasa baada ya kifo cha Audax, aliyebakia hai ni mmoja tu Nguza Viking ambaye nae yuko kifungoni akitumikia adhabu ya kifungo cha maisha. Mzee Audax alianza matatizo yake ya kiafya mwaka 2005 baada ya kupata stroke iliyomfanya apooze upande mmoja wa mwili. Amekuwa akilelelwa na wanae kwa muda wote huo kutokana na kutoweza kuendelea na kazi kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Baadhi ya nyimbo alizotunga marehemu ni Kisebengo, Mpenzi Luta, Mimi na nyingi sana nyinginezo. Angalia video ya Maquis Original Audax alipokuwa kijana
MUNGU AMLAZE PEMA AUDAX
Katika Kipindi cha ZAMA ZILE EFM 93.7fm siku ya Jumapili kuanzia saa mbili hadi saa tano usiku kutakuweko na maelezo mengi zaidi kuhusu Mzee Audax na bendi yake ya Maquis Du Zaire
Comments
Post a Comment