Msuva agoma kujiunga Simba SC


Msuva agoma kujiunga Simba SC
NgassanaMsuva
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Msuva amekuwa akiwatoa udenda vigogo wa Simba kutokana na mafanikio yake katika klabu ya Yanga.'
MKALI wa mabao kwa sasa katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), winga mzawa Simon Msuva wa Yanga SC, amesema hana mpango wa kujiunga na watani wao wa jadi, Simba SC.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hanspope, aliweka wazi Desemba mwaka jana kuwa klabu hiyo ya Msimbazi, iko mbioni kupeleka ofa Yanga SC ili wamwachie mkali huyo wa mabao.
Hata hivyo, mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Police Moro FC waliyoshinda 4-1 na kutwaa taji la 25 la Tanzania Bara katika Uwanja wa Taifa jijini hapa jana, Msuva alisema hajazungumza na kiongozi yeyote wa Simba SC na hana mpango wa kuihama Yanga SC kwa sasa.
"Ni stori tu ambazo zipo mitaani kwamba mimi niakwenda Simba. Sijazungumza na kiongozi hata mmoja wa Simba kuhusu suala hilo na kwa sasa sina mpango wa kuondoka Yanga," alisema Msuva.
Alipoulizwa kuhusu kuwa na mapenzi na Simba inavyodaiwa na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo ya Msimbazi, Msuva alisema: "Sijazaliwa na Simba, nimezaliwa na Mzee Msuva." 
Winga huyo hatari aliyekulia Azam FC kisha kutimkia Moro United kabla ya kutua Yanga SC 2012, amefunga mabao 17 VPL msimu huu ikiwa ni mawili pungufu ya mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe aliyofunga msimu uliopita na kutwaa kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora.


Comments