LIVERPOOL KUPITISHA PANGA KALI, WACHEZAJI 10 KWENDA NA MAJI …wamo Balotelli, Glen Johnson, Kolo Toure, Lambert na Fabio Borini



LIVERPOOL KUPITISHA PANGA KALI, WACHEZAJI 10 KWENDA NA MAJI …wamo Balotelli, Glen Johnson, Kolo Toure, Lambert na Fabio Borini

LIVERPOOL inaelezwa itapitisha panga kufyeka wachezaji wake 10 kiangazi hiki wakati Brendan Rodgers akitaka kusuka upya kikosi chake baada ya kuhakikishiwa kubaki.
The Reds imeshindwa kuendeleza makali yake ya msimu uliopita ilipokuwa ikipigania taji la Premier League na kwa sasa inashika nafasi ya tano, ikiachwa pointi saba nyuma ya mstari wa tiketi ya Champions League.
Liverpool ililazimika kutumia fedha nyingi baada ya Kombe la Dunia kufuatia kuondoka kwa Luis Suarez aliyekwenda Barcelona, lakini wakali kama Mario Balotell na Rickie Lambert wameshindwa kukidhi haja.
Gazeti la Daily Mail limedai nyota 10 watakaoondoka mwisho wa msimu ni pamoja na Steven Gerrard ambaye tayari amethibitishwa kuhamia LA Galaxy ya Marekani.
Glen Johnson na Kolo Toure wanatarajiwa kuwa huru baada ya mikataba yao kufika mwisho, wakati Javi Manquillo hatapewa mkataba wa kudumu baada ya kucheza kwa mkopo.
Washambuliaji Balotelli, Lambert na Fabio Borini wanatajwa kufunguliwa mlango wa kutoka Anfield sambamba na Brad Jones, huku Martin Skrtel ambaye hajasaini mkataba mpya akiwa na uwezekano wa kuuzwa Wolfsburg, wakati Raheem Sterling akifukuziwa na Manchester City, Chelsea na Arsenal.


Comments