Licha ya kutwaa ubingwa Pluijm bado ana mzuka wa kuvuna pointi



Licha ya kutwaa ubingwa Pluijm bado ana mzuka wa kuvuna pointi

Kocha

KOCHA mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van der Pluijm 'Babu' amesema kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kumempa faraja kubwa na sasa anaelekeza nguvu zake kwenye mechi ya marudiano ya kombe la shirikisho dhidi ya Etoile du Sahel itayopigwa mwishoni mwa wiki hii nchini Tunisia.

"Siku zote nashangazwa na mashabiki wa Yanga, wananiunga mkono kwa kiwango cha juu, nafurahia sana maisha ya soka Tanzania, nimechukua ubingwa wangu wa kwanza baada ya kushindwa mwaka jana, hii ni hatua nzuri kwangu na sasa naelekeza nguvu zangu kwenye mechi ya kimataifa dhidi ya Etoile". Amesema Pluijm na kuongeza: "Tulitoka sare ya 1-1, katika mpira lolote linaweza kutokea, tutaenda kucheza kwa kushambulia, lazima tupate magoli".

Aidha, Pluijm amesisitiza kuwa anahitaji kushinda mechi mbili zijazo za ligi kuu dhidi ya Azam fc na Ndanda fc ili kunogesha zaidi ubingwa.

"Ligi ni ngumu, timu zinacheza kwa nguvu, nimebakiwa na mechi mbili, lazima tushinde, hatuna mzaha hata kidogo". Amesema Pluijm.

Ushindi wa Yanga wa magoli 4-1 waliopata dhidi ya Polisi Moro umewafanya wafikishe pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Azam wamebakiza mechi tatu, Yanga mbili, lakini wakishinda zote wanalambalamba watafikisha pointi 54 kutoka 45 walizokusanya mpaka sasa katika nafasi ya pili.



Comments