Kukosekana kwa uzalendo ni chanzo cha timu za mikoani kufanya vibaya ligi kuu


Kukosekana kwa uzalendo ni chanzo cha timu za mikoani kufanya vibaya ligi kuu

standd

Stand United wameshika roho mkononi wakisikilizia usalama wa kubaki leigi kuu

Na Shaffih Dauda

WASWAHILI 'wanasema mbio za sakafuni huishia ukingoni', hakuna jambo lenye mwanzo likakosa mwisho wake, hatimaye ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015 inaelekea saa za magharibi.

Timu chache zimebakiwa na michezo mitatu, lakini nyingi zimesaliwa na karata mbili tu kujua hatima ya kubaki au kwenda na maji.

Ligi ya msimu huu inasemekana kuwa na changamoto kubwa ya kiushindani, watu wengi wanaangalia namna timu zinavyofungana pointi, kama kigezo ni hicho tu,  basi kweli ushindani umeongezeka.

Tanzania Prisons wanashika mkia kwa kujikusanyia pointi 25 kufuatia kucheza mechi 24, lakini wanatofautiana pointi 6 tu na timu zinazoshika nafasi ya nne (Mbeya City) na tano (Kagera Sugar) zenye pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 24.

Kwa mazingira hayo, Prisons wanaweza kubaki ligi kuu kama watafanya vizuri kwenye mechi mbili zilizosalia ikiwemo ile ya mahasimu wa jiji la Mbeya dhidi ya Mbeya City fc.

Si jambo la kawaida kuwa na timu 10 kwenye msimamo zisizokuwa na uhakika wa kubaki ligi kuu, ni ligi ya aina yake na kila timu roho inadunda.  Hakuna tena faida ya kucheza nyumbani, timu zinapambana kusaka pointi tatu, mfano jana Mtibwa Sugar walikufa kwao goli 1-0 dhidi ya JKT Ruvu.

Licha ya ushindani huo, Yanga wanaweza kumaliza kazi leo kama wataifunga Polisi Morogoro uwanja wa Taifa Dar es salaam kwasababu wanahitaji pointi tatu tu kufikisha 55 ambazo haziwezi kufikiwa na mabingwa watetezi Azam fc hata kama watashinda mechi zao zote tatu zilizobakia.

Yanga wana pointi 52 baada ya kucheza mechi 23 wakifuatiwa na Azam fc wenye pointi 45 baada ya kucheza mechi 23, kama Azam watashinda mechi tatu zilizosalia watafikisha pointi 54 ambazo Yanga watakuwa wamevuka kama wataibuka kifua mbele jioni ya leo.

Kwa asilimia kubwa, Simba wanaoshika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 41 baada ya kucheza mechi 24 watamaliza ligi katika nafasi hiyo kama watashinda mechi zao mbili zilizosalia, ni ngumu sana Azam fc kuzidiwa na Mnyama ingawa lolote linaweza kutokea.

Tuweke kando hayo na sasa tuangalia kile nilichokusudia kusema leo hii kutokana na utafiti uliofanywa na mtandao huu kuhusu timu za mikoani kufanya vibaya ukitumia klabu mbili za Stand United na Ndanda fc.

Hizi ni timu mbili za wananchi kama ilivyo kwa Simba na Yanga, zinagusa maisha ya watu wa kawaida mno ukilinganisha na timu za majeshi kama vile JKT Ruvu, Ruvu Shooting pamoja na timu za makampuni kama vile Azam fc, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Ndanda na Stand United hazina matokeo mazuri  msimu huu ambao ni wakwanza kwao, zipo katika mstari mwekundu. Mpaka sasa, Stand wamebakiwa na michezo miwili kumaliza msimu wakiwa na pointi 28 katika nafasi ya 10, wakati Ndanda nao wamebakiwa na michezo miwili wakiwa tayari wamekusanya pointi 25 katika nafasi ya 12.

Ndanda fc hali ni tete

Kwa mfano tuichambue Ndanda fc; klabu hii imeshinda mechi tatu (3) nyumbani na tatu (3) ugenini, imepoteza mechi 8 ugenini na tatu nyumbani. Imetoa sare sita (6) nyumbani na moja ugenini.

Ukiyatazama matokeo haya unaona haijafanya vizuri uwanja wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona, sehemu ambayo wangetengeneza matokeo mazuri.

Swali linakuja, kwanini timu nyingi za mikoani za wananchi zinafanya vibaya ligi kuu?

Majibu yanaweza kuwa mengi, lakini utafiti uliofanywa na mtandao huu umebainisha kuwa sababu iliyobeba uzito wa  juu ni kukosekana kwa uzalendo, kumbuka utafiti huu haujafungwa, mtu yeyote anaweza kutoa sababu zake.

Ndanda fc ina wachezaji watatu tu wanaotoka Mikoa ya kusini ambao ni Omari Nyenye kutoka Mtwara, Salum Mineli kutoka Newala na Majidi Lubanda kutoka Lindi. Kwa maana hiyo wanaotoka Mtwara ni wawili tu na hiyo ni timu ya wananchi wa Mtwara.

Lakini ukiangalia wakati ule timu ya Bandari Mtwara iliundwa na wachezaji wengi wazawa wa mkoa huo wakiwemo Mohamed Hussein 'Chinga', Hassan Ahmed, Shomari Seleman, Andrew Nyambi, David Anawake, Amlima, Said Mnunduma, Liziga, Yusuf Jeta, Jerome Gabriel, Jacob Peter, Ziada Ambunda.

Hii ilikuwa na faida kubwa moja, walicheza kwa uzalendo, waliitetea timu yao, walijitolea kwa nguvu zote, walikuwa na utashi wa kujua wananchi wanataka nini, waliweka maslahi pembeni, walitetea nembo ya timu yao tofauti na ilivyo kwa Ndanda iliyojaza wachezaji wengi kutoka nje ya mkoa.

Ukiitazama timu ya Stand United, 'Chama la Wana', ina wachezaji wachache wazawa kama vile David Mwita, Pastory Athanas, , Richard Elisha, Ganga John, Jisend Mathias. Walio wengi wanatoka nje ya Shinyanga, hebu angalia walichofanya Shabani Kondo, Hamis Thabeet na Patrick  Mrope, wachezaji hawa waliikimbia timu kwa kukosa uzalendo na hii ni kwasababu ya kutokuwa wazawa.

Ukirudisha kumbukumbu nyuma, timu ya wakati ule, RTC Shinyanga ilikuwa na wachezaji wengi wazawa , mfano, Abadallah Magubika, Paul John Masanja, Deus Pamba, Willy John, Charles Masule, Mwinyimvua Komba, Musa Salum, Nchambi Juma, Joseph Lubisha.

Siku hizi hakuna tena 'programu' ya kuzalisha wachezaji wazawa kwa timu za mikoani na hili ndio chimbuko la timu hizi kufanya vibaya, wachezaji wanaosajiliwa kutoka nje ya mikoa hiyo wanakosa uzalendo.

Kwa utaratibu ulivyo duniani,  asilimia kubwa ya wachezaji wanaounda timu za miji wanatakiwa kuwa wazawa ili wapambane na kupata matokeo, lakini kwa timu za Ndanda na Stand hazina wazawa, wachezaji wengi  ni wageni, wanakuja kutafuta maslahi.

Inapotokea timu hazijawalipa mishahara mwezi mmoja au miwili, wachezaji wanakosa uzalendo, hawachezi vizuri kwasababu hakuna wanachopoteza kama timu itashuka wataondoka zao na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

Wakati utafiti huu unafanyika, ilielezwa kuwa timu ya Kariakoo ya Lindi, wakati inacheza ligi kuu, kocha wake Salum Madadi alikuwa na uwezo wa kupanga wachezaji wote wa Lindi.

Na mara zote kwenye mechi za nyumbani,  Madadi alikuwa anapanga wachezaji wengi wazawa, mashabiki wakienda uwanjani wanawaona wana wao, washikaji zao na  hii iliwafanya wachezaji wajitolee, maslahi hayakupewa kipaumbele, walipambana  kwa ajili ya timu yao ya nyumbani tofauti na siku hizi, hakuna morali ya hivyo.

Unapokuwa na wachezaji wengi waliokuja kuvuna pesa kupitia mpira lazima uwalipe ili wacheze vizuri, lakini ukikwama kidogo kifedha watacheza vibaya. Timu nyingi za wananchi hazina uwezo wa kifedha, kuna wakati zinakwama kulipa posho, mishahara kwasababu wakati fulani zinategemea misaada ya wananchi wenyewe ingawa siku hizi kuna wadhamini tofauti tofauti.

Kinachotakiwa kufanyika ili kurudisha hadhi ya timu za mikoani ni kuwa na mpango maalumu wa kuzalisha wachezaji wazawa, sio vibaya kusajili kutoka nje ya mkoa, lakini angalau asilimia 60-70 wawe wazawa ambao watamwaga mpaka tone la mwisho kupigania timu zao.

Nawatakia jumatatu njema! Tukutane tena jumatano panapo majaaliwa!



Comments