'Simba na Azam FC ndizo timu pekee zenye uwezo wa kumaliza katika nafasi ya pili.'
KOCHA mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kapunovic, ametamba kuwa timu yake itaibuka na ushindi Jumamosi wakati watakapocheza dhidi ya Azam katika Uwanja wa Taifa jijini hapa na kuweka hai matumaini yao ya kumaliza nafasi ya pili msimu huu.
Azam FC inayonolewa na Mganda George 'Best' Nsimbe iko nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi 45, 10 nyuma ya mabingwa Yanga na nne mbele ya Simba ambao wako nafasi ya tatu wakiwa wamecheza mechi 24, moja zaidi ya Azam.
Kopunovic ameiambia mtandao huu leo jijini hapa kuwa wanaitaka nafasi ya pili na ili lengo lao lifanikiwe lazima waifunge Azam katika mchezo huo kutimiza lengo lao.
"Tunataka kushiriki michuano ya kimataifa na njia pekee ya kuipata nafasi hiyo ni kuifunga Azam. Ninajua siyo kazi ndogo, lakini hakuna kinachoshindikana kutokana na maandalizi tuliyofanya," amesema Kopunovic.
Simba na Azam FC zinagombania nafasi ya pili katika msimamo wa ligi zikitofautina kwa pointi nne, huku kila mmoja ikionyesha shauku ya kutaka kushinda katika mchezo huo ili kushiriki katika michuano ya kimataifa mwakani.
Comments
Post a Comment