Band maarufu kutoka Morogoro, iliyoanza katika miaka ya arobaini kwa jina la La Paloma na mwaka 1952 ikaanza kuitwa Cuban Marimba, jana 26 April 2015 ilitunukiwa Nishani ya miaka 50 ya Muungano kutoka kwa Rais wa jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dr. Jakaya Kikwete. Beni hii ilitokea wapi? Pata uhondo hapa.
Cuban Marimba Band 
          Morogoro,              moja ya miji iliyokuwa maarufu kwa burudani katika miaka ya              hamsini, sitini na sabini. Watu walitoka Dar es Salaam na              kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa              bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya              wafanyakazi watake kupangwa kituo cha Morogoro. Kati ya hizo              bendi mbili, ilkuweko Cuban Marimba Band. Bendi hii ilikuwa              ndoto ya mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama              SAY. Salum Abdallah alizaliwa tarehe 5 Mei, mwaka 1928. Baba              yake alikuwa mwarabu na mama yake mwenyeji wa Morogoro..              Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa              kuendelea na shule Dar es Salaam , maana wakati ule              ililazimika kuja Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada              ya hapo.  Pamoja na kufaulu huko baba yake aliamua abakie              nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara. Katika              kipindi hiki Salum alianza kuonyesha kupenda kwake muziki.              Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa              kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika. Pamoja na              baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda              mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya kupigia hizo              santuri. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende              Cuba kujifunza muziki. Alitoroka hadi Mombasa ili apande              meli kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na              vuguvugu la vita ya pili ya dunia na safari yake ikaishia              Mombasa.  Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia              mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka              wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa              sana na vifaa vya Dar Es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye              na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na              vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita              bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo              mmoja katika santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha              kwamba mpaka leo bado inapigwa duniani kote, na hata              kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Elvis Presley              aliyeingia katika anga za muziki baadae sana.  La Paloma ,              ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein-              Mweka hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu              Katibu Mkuu, Salum Abdallah –Band Master.
          Katika              kuiona Dar Es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama              vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri              nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar              Es Salaam Jazz band. Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi.              Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar              Hussein-Mweka Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki              walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo,Mgembe,Juma              Kondo,Nzige, Daulinge. Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina              la Cuban Marimba Jazz Band. Kundi lilianza kuwa maarufu              kiasi cha kuwa mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri              Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi nyimbo za bendi              hii.  Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka              ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo              taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na              gari lake likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka              kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa tarehe 19 Novemba              1965.
          (Picha                kwa hisani ya Jumaa R. R. Mkabarah) 
        
Comments
Post a Comment