CARLO ANCELOTTI ASEMA HAWANA HARAKA NA USAJILI WA JAVIER HERNANDEZ CHICHARITO


CARLO ANCELOTTI ASEMA HAWANA HARAKA NA USAJILI WA JAVIER HERNANDEZ CHICHARITO

Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema hana haraka juu ya hatima ya mshambuliaji Javier Hernandez Chicharito licha ya kuonyesha kiwango cha juu katika mechi za hivi karibuni.
Chicharito aliitumia vizuri nafasi aliyoipata hivi karibuni baada ya Karim Benzema kuwa majeruhi, kwa kufunga bao la dakika za mwisho wakati Madrid ikiichapa Atletico Madrid 1-0 katika robo fainali ya Champions League kabla kufunga mara mbili katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Celta Vigo Jumapili iliyopita.
Raia huyo wa Mexico anayecheza Madrid kwa mkopo kutoka Manchester United, ameonyesha uwezo wake kwa vitendo wakati akiwachezea mabingwa hao wa Ulaya, lakini Ancelotti yuko tayari kusubiri hadi mwisho wa msimu kabla kuamua kujaribu kumbakisha moja kwa moja Santiago Bernabeu ama vinginevyo.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Ancelotti alisema: "Hatma ya Chicharito itafanyiwa tathmini mwisho wa msimu. Nimependa kazi yake mwaka wote, na wakati alipopata nafasi aliitumia vizuri. Kwa kocha kuwa na wachezaji ambao wako tayari daima ni jambo zuri.
"Kila mmoja ana furaha na Chicharito. Natumaini atabaki kwa njia hiyo."



Comments