Mayaula Mayoni alizaliwa tarehe 6 November 1946 katika jiji la Léopoldville, ambalo sasa linaitwa Kinshasa. Alimaliza shule za awali bila matatizo na kumaliza elimu ya sekondari mwaka1962 katika Chuo cha Kisantu. Alipenda sana mpira na kati ya mwaka 1968 na 1971 alicheza nafasi ya winga wa kushoto katika timu ya 'AS Vita Club' ya Kinshasa, na aliweza kuchaguliwa hata timu ya Taifa ya nchi yake. Baba yake alipopata nafasi ya kufanya kazi katika Ubalozi wa Zaire nchini Tanzania, Mayaula alimfuata huku na kujiunga na timu ya Young Africans. Aliondoka Dar es salaam na kuelekea jiji la Charleroi, Ubelgiji alikokwenda kujiendeleza kimasomo katika kozi ya Data Processing. Akajiunga na timu za mpira ya 'Racing Club de Charleroi' baadae akajiunga na 'Racing Club de Jette' ya Brussels. Kwa muda mfupi alichezea timu ya 'FC ya Fribourg ya Swtzerland, na ni katika kipindi hiki alipoanza kujifunza kupiga gitaa, na muda si mrefu akajiunga na bendi ya wanafunzi wa Kikongo iliyoitwa Orchestra 'Africana' akiwa kama mpiga rhythm gitaa.
Aliporudi Kinshasa, Mayaula akabadili kazi kutoka kwenye mpira na kuwa mwanamuziki mtunzi, hakuchukua muda mrefu akagunduliwa na Franco aliyemtaka Mayaula kujiunga na TP OK Jazz, na ndio wakati huo Mayaula akatoa kibao cha Cherie Bondowe. Wimbo huu ulipokelewa vizuri sana na wapenzi wa muziki lakini National Censorship Commission ya Zaire wakati huo, iliupiga marufuku kwa kuwa ulikuwa ni wimbo ambao hadithi yake ilikuwa ni changudoa mmoja aliyekuwa akielezea shughuli zake zilivyo, Commission iliona wimbo unatetea uchangudoa na hivyo kuupiga marufuku. TP OK Jazz ililzazimika kuusambaza kutokea Ubelgiji na hatimae ukaenea Kongo na sehemu nyingine za Afrika. Inasemekana kuwa japo Franco alimkaribisha OK Jazz, hakuwahi kuwa mwanachama halisi wa kundi hilo kwani alipendelea kuwa huru kutunga nyimbo zake, na kumpa msanii aliyemtaka. Tungo zake kadhaa zilifanyiwa kazi na TP OK Jazz kama vile Nabali misere na Moni.
Mwaka 1977 tungo yake iliyoitwa Ndaya ilichukuliwa na kuimbwa na mwanamuziki Mpongo Love, wimbo huo ulikuwa unaongea kuhusu mwanamke aliye na furaha kutokana na kuwa na mume bora na kuweza kumbana mumewe kutoka kwa wanawake wengine. Mwaka 1981 Mayaula aliondoka Zaire akiwa na wanamuziki kutoka bendi ya Abeti Masikini na kuhamia Afrika Magharibi ambako kati ya mwaka huo na 1984 alirekodi album kadhaa chini ya label ya Disc-Oriënt ya Lome Togo. Mwaka 1984 alirudi Zaire na mwaka 1986 alitoa album iliyoitwa 'Fiona fiona', na mwaka huohuo Tshala Muana alipata umaarufu kutokana na wimbo 'Nasi nabali', uliotungwa na Mayaula Mayoni. Baada ya hapo akarekodi album yake Mizele akiwa na TP OK Jazz wakisindikizwa na waimbaji Carlito Lassa and Malage de Lugendo.
Mwaka 1993 alitoa album ya 'L'amour au kilo' na miaka saba baadae akatoa album nyingine 'Bikini'. Baada ya album hii Mayaula alihamia Dar es Salaam na kuanza kufanya kazi ubalozi wa Kongo. Muda si mrefu akaanza kuugua na kuamua kurudi Makadi, kwao alikozaliwa. Hali yake ilizidi kuwa mbaya mwaka 2005 akapelekwa Ubelgiji kwa matibabu na hatimae kufariki Brussels May 26, 2010 akiwa na umri wa miaka 64. Katika maisha yake alichaguliwa mtunzi bora wa Zaire 1978 kwa wimbo Bondowe 2, mwaka 1979 kwa wimbo Nabali Misere na mwaka 1993 'Ousmane Bakayoko'.
Comments
Post a Comment