Tenga: CAF, CECAFA zinamuunga mkono Blatter urais FIFA


Tenga: CAF, CECAFA zinamuunga mkono Blatter urais FIFA

2Na Berha Lumala, Dar es Salaam
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yameungana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kumpigia upatu Rais wa FIFA, Sepp Blatter katika uchaguzi mkuu ujao wa shirikisho hilo la kimataifa.

Uchaguzi wa Rais wa FIFA umepangwa kufanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka ulimwenguni utakaofanyika Zurich, Uswisi Mei 28-29, mwaka huu na Kamati ya Uchaguzi ya FIFA imempitisha Blatter na watu wengine watatu akiwamo kiungo nguli wa zamani wa Urono, Luis Figo kuwania kiti hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya TFF jijini hapa leo, Rais wa CECAFA na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Leodegar Tenga, amesema baraza hilo linaunga mkono msimamo wa Bara la Afrika uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika mwaka jana jijini Sao Paulo, Brazil kuwa wanachama wote wa CAF watamuunga mkono Rais wa sasa wa FIFA, Blatter kutetea nafasi yake katika uchaguzi ujao.

Aidha, Tenga ambaye aliwahi kuwa rais wa TFF, ametumia fursa hiyo kuishukuru familia ya TFF kwa kumuunga mkono katika kugombea tena nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF katika uchaguzi ujao utakaofanyika Aprili 7-8, mwaka huu jijini Cairo, Misri. Tenga ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati baada ya mpinzani wake kujitoa.

"Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika Desemba 2014 jijini Nairobi, Kenya ulipitisha azimio la kumuunga mkono Sepp Blatter katika uchaguzi mkuu ujao wa FIFA. Nikiwa Mwenyekiti wa CECAFA, niko hapa leo kusisitiza msimamo wetu huo," Tenga amesema na kuongeza:

"Blatter amekuwa mbele kuunga mkono maendeleo ya soka kwa nchi changa hasa barani Afrika. Amesimama imara pia kupinga ubaguzi katika soka. Afrika imeona anatufaa."

Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ambaye alikuwa amefuatana na Tenga katika mkutano na waandishi wa habari leo, ametoa tamko rasmi kuwa TFF atampigia kura Blatter katika uchaguzi ujao.



Comments