Samatta aeleza sababu Stars kubanwa na Malawi


Samatta aeleza sababu Stars kubanwa na Malawi

SamattaMshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samatta, ametoa siri ya kutofanya vizuri kwa Taifa Stars dhidi ya timu ya taifa ya Malawi katika mechi yao iliyopita.

Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana huku mchezaji huyo wa zamani wa African Lyon FC na Simba SC akiinusuru Stars kulala nyumbani kwa kufunga bao la kusawazisha katika robo saa ya tatu ya mchezo.
Samatta ameuambia mtandao huu kuwa nyota wa Malawi 'The Flames' wanaijua vyema Taifa Stars ndiyo maana waliwabana vilivyo baadhi ya wachezaji hatari wa Tanzania.

"Tumecheza dhidi ya Malawi zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi kifupi, wanatujua mbinu zetu ndiyo maana walimbana sana (Thomas) Ulimwengu na wachezaji wetu wengine wenye waliowaona kuwa tishio kwao," Samatta amesema.

"Naamini tungecheza dhidi ya timu ambayo haitujui, tungepata matokeo mazuri.  Tulijiandaa kushinda, lakini nao walijipanga kupata matokeo mazuri ugenini. Inakuwa ngumu kucheza dhidi ya timu ambayo inafahamu vyema mbinu zako."

Taifa Stars ilicheza dhidi ya Malawi mara mbili mwaka jana katika mechi za kirafiki zilizochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya na Uwanja wa Taifa jijini hapa.



Comments