ROGART HEGGA: MASHUJAA BAND HAMTAJUTIA KUNISAJILI …aahidi mambo mazito, Chaz Baba naye asema sasa timu imetimia
Mwimbaji na mtunzi nyota wa muziki wa dansi, Rogart Hegga (pichani juu) ambaye amejiunga na Mashujaa Band, amesema kamwe bendi hiyo haitajuta kumchukua kutokana na mambo matamu atakayoyashusha kwenye 'ofisi' yake hiyo mpya.
Hegga ameahidi kutowaangusha mashabiki wa bendi hiyo na mashabiki wake binafsi ambao wanakubali uwezo alionao kwenye sanaa hiyo.
Mwimbaji huyo akaongeza kuwa ameamua kujiunga na Mashujaa kwa sababu anataka kufanya kazi katika bendi yenye wasanii wenye uwezo ambapo kwa pamoja watatumia vipaji vyao kutengeneza kazi zenye akili.
"Nimekuja kuongeza chachu, nimejiunga Mashujaa kwa sababu nafahamu wasanii walioko kwenye bendi hii ni bora, naahidi kuwapa furaha mashabiki wa bendi hii, hawatajutia ujio wangu ndani ya Mashujaa", alisema mwanamuziki huyo ambaye amewahi pia kufanya kazi katika bendi ya Mchinga Sound African Stars 'Twanga Pepeta' TOT Band na Extra Bongo.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Mashujaa, Maximilian Luhanga, alisema kuwa watamtambulisha Hegga katika onyesho maalumu litakalofanyika Aprili 5 siku ya Pasaka.
Luhanga alisema kuwa ujio wa msanii huyo utaongeza changamoto kwenye bendi yao ambayo imepanga kufanya makubwa zaidi kwenye kwenye soko la muziki wa dansi.
Akizungumzia ujio wa mwanamuziki huyo Rais wa bendi hiyo Charles Gabriel 'Chaz Baba Kingunge' alisema kwamba amefurahia ujio wa Hegga ambaye anamuamini na kuufahamu uwezo wake wa kazi.
"Moyo wangu umejaa furaha huku nikiamini kuwa sasa timu imetimia. Nasema karibu sana Mashujaa, najua uwezo wangu na wako utatoa matunda mazuri" alisema Chaz.
Moja ya nyimbo ambazo zilipata umaarufu na kutamba zilizotungwa na Hegga ni "Fadhila kwa Wazazi" ambayo aliiandaa akiwa na Twanga Pepeta na baadae kutunga sehemu ya pili ya wimbo huo akiwa na Mchinga Sound.
Comments
Post a Comment