Na Augustino Mabalwe,Dar es salaam.
Kiungo wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani Mesut Ozil amesema miaka ijayo anaamini atashinda tuzo ya Ballon d'or na jinsi wachambuzi wanavyozidi kumkosoa ndiyo anapata nguvu ya kujituma zaidi.
Mjerumani huyo ameichezea Arsenal mechi 14 tu katika ligi kuu msimu huu kufuatia kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha lakini tangu arudi tena uwanjani amekuwa katika kiwango bora.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Real Madrid anaonekana kuizoea ligi ya Uingereza tofauti na hapo awali. "Nikiendelea kufanya vizuri, afya yangu ikawa imara basi miaka michache ijayo Ballon d'or itakuwa mikononi mwangu" alisema Ozil. ."Ninajisikia vizuri. Mimi ni mchezaji mkubwa duniani,ninacheza katika klabu kubwa. Pia hii ligi tunatumia nguvu nyingi kuliko kule La Liga kwa hiyo ninazidi kuimarika zaidi kuliko mwanzo " aliongeza Ozil.
Pia mchezaji huyo amesema kitendo cha kiungo wa zamani wa Manchester United Paul Scholes kuponda kiwango chake kilimuongezea nguvu ya kupambana na kuongeza kujituma zaidi.
Ozil sasa yupo katika majukumu ya timu ya taifa ya Ujerumani ambao jumapili watashuka dimbani kuwavaa Georgia katika mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu michuano ya mataifa Ulaya yatakayofanyika mwaka 2016 nchini Ufaransa.
Comments
Post a Comment