Mfalme wa taarab hapa nchini, Mzee Yussuf ameiambia Saluti5 kuwa safari hii atapiga gitaa la bass katika baadhi ya nyimbo mpya za albam ijayo ya Jahazi Modern Taarab.
Wengi wamemzoea Mzee Yussuf kama mtunzi, mwimbaji na mpiga kinanda, lakini sasa nyota huyo anasema ni wakati wa kuwaonyesha watu kipaji chake kingine.
"Nina uwezo kupiga gitaa la bass na nimekuwa nikifanya hivyo katika maonyesho yetu, lakini sasa umefika wakati wa kushiriki kikamilifu katika chombo hicho hasa wakati wa kurekodi," anasema Mzee Yussuf.
Jumapili iliyopita Saluti5 ilimshuhudia Mzee Yussuf akilikung'uta gitaa hilo kwa ufasaha kwenye onyesho la bendi yake pale Travertine Hotel.
Mzee Yussuf anasema wakati mwingine kero na usumbufu wa wasanii unamfanya apate ari ya kujifunza vitu vingi katika muziki. "Kwa sasa nina uwezo wa kupiga kila chombo kwenye taarab," anafafanua Mfalme Mzee Yussuf.


Comments
Post a Comment