‘Msuva, Tambwe wanafunga tu, pointi 18 ugenini, mwisho wa Yanga ni nini…’



'Msuva, Tambwe wanafunga tu, pointi 18 ugenini, mwisho wa Yanga ni nini…'

msuva yangaNa Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

Tayari mshambulizi, Mrundi, Amis Tambwe amefunga magoli saba katika klabu ya Yanga SC tangu aliposajiliwa kwa ' usajili wa kushtukiza' siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo, 15 Disemba, 2014 baada ya kutupiwa virago na klabu ya Simba SC wakati wa utawala wa Patrick Phiri. Yanga ilitanua wigo wa pointi kileleni mwa msimamo baada ya ushindi wa kuvutia ugenini, Mkwakwani Stadium, Tanga dhidi ya JKT Mgambo ( timu ambayo ilikuwa haijapoteza katika uwanja wake msimu huu).

Katika mchezo huo ambao Yanga walishinda kwa mabao 2-0 ( ushindi wa sita ugenini msimu huu, Stand United 0-3 Yanga, Polisi Morogoro 0-1 Yanga, Coastal Union 0-1 Yanga, Tanzania Prisons 0-3 Yanga, Mbeya City 1-3 Yanga, Mgambo 0-1 Yanga ). Sitaki kuzungumzia ubora wa mchezaji mmjo mmoja kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuwakosea heshima wachezaji wote wa Yanga kuanzia kwa golikipa, Ally Mustapha.

Walinzi,  Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Edward Charles, Kelvin Yondan, Rajab Zahir, Nahodha, Nadir Haroub, Said Juma ' Makapu', Salum Telela, Hassan Dilunga, Mrisho Ngassa, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Andrey Coutinho, Nizar Khalfan, Jeryson Tegete, Hussein Javu ambao walikuwa na timu hiyo tangu ikiwa chini ya Marcio Maximo.Mbuyu Twite

Wachezaji waliosajiliwa wakati wa dirisha dogo pia wamekuwa na mchango mkubwa, Danny Mrwanda ndiye aliyefunga bao pekee katika ushindi mgumu dhidi ya Polisi Moro katika uwanja wa Jamhuri , Danny amekuwa na msaada si katika gemu moja tu bali katika michezo yote aliyopewa nafasi amefanikiwa kufanya vizuri,.

Tambwe amefunga mabao manne katika ligi kuu tangu alipojiunga na Yanga na mabao matatu katika michezo mitatu ya Kombe la Shirikisho Afrika, msaada wake haupo katika kufunga tu, amekuwa akishuka hadi maeneo ya katikati ya uwanja kutafuta mipira na kukaba wapinzani wake timu inapozidiwa, ni mchezaji anayejituma zaidi kwa sasa katika safu ya mashambulizi ya Yanga huku akitumia vizuri nafasi anazotengenezewa.

 tambwe+pichaTambwe anategemea zaidi timu icheze ili afunge mabao, haijalishi ni mipira ya namna gani anapasiwa iwe ya juu au ile ya chini. Alifunga goli maridadi sana mbele ya golikipa ' mjanja mjanja' Godson Mmasa baada ya kuruka juu na kupiga kiki ya kichwa akiunganisha krosi ya Msuva. Lilikuwa bao la pili kwa Yanga na liliwazima kabisa Mgambo. Huu ni usajili bora zaidi katika dirisha dogo la pengine Yanga walikuwa na bahati kwa kuwa walikumbuka namna Tambwe alivyo wanyanyasa walinzi wa timu pinzani katika msimu wake wa kwanza tu katika ligi kuu ya Bara ambao alitwaa ufungaji bora kwa rekodi ya mabao 19 katika michezo 23.

 Amefunga magoli yote manne ya Yanga kwa mipira ya kichwa katika ligi kuu. Ni mkali wa kuvizia na kutumia makosa ya walinzi wa timu pinzani. Yanga ambayo kwa sasa mfungaji wake bora ni Msuva inashangaza nap engine inafurahisha sana kwa namna inavyocheza kama ' timu kubwa', timu yenye malengo makubwa katika kila mchezo. Kpah Sherman unaweza usione msaada wake kwa sasa kwa kuwa hafungi, lakini Yanga wanaendelea kusonga mbele katika michuano ya Afrika bila shaka kuna kitu anaweza kulipa kwa klabu yake.

Ushindi wao ugenini umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mbinu za mwalimu Hans Van Der Pluijm ambaye tangu amechukua timu hiyo mwishoni mwa mwaka uliopita amepoteza michezo miwili tu( 2-1 ugenini dhidi ya BDF IX ya Botswana, Simba 1-0 Yanga katika ligi kuu). Kila mtu alitegemea baada ya timu hiyo kupoteza dhidi ya Simba ingesambaratika na kukosa uelekeo, lakini saikolojia nzuri iliyojengwa kwa wachezaji iliwafanya kusahau matukio yote yaliyotekea katika ' Dar es Salaam derby' na kuzisambaratisha Platinum FC ya Zimbabwe kwa mabao 5-1 katika michuano ya Shirikisho, kisha kuzifunga timu ngumu za Kagera Sugar na JJK Mgambo katika ligi kuu. 

Kushinda michezo sita kati ya nane ya ugenini msimu huu ni dalili za mafanikio, Msuva amekuwa kinara wa ufungaji katika timu huku akifunga magoli manne ugenini kati ya tisa aliyofunga hadi sasa katika ligi kuu. Kiwango kizuri cha sasa kutoka kwa Ngassa ni kielelezo kingine kuwa timu hiyo inaendelea kuamka na kuhitaji kurudisha ubingwa waliopoteza mbele ya Azam FC msimu uliopita.

Wakiwa na alama 37 katika michezo 18, alama moja mbele ya Azam, Yanga wanawastani wa mabao mawili zaidi ya mabingwa hao watetezi ambao wamefunga mabao ya kufunga ( wote wakiwa na mabao 25) Yanga wameruhusu nyavu zao mara kumi tu wakati AZam FC wamefanya hivyo mara 12.

 Kama safu ya ulinzi itaendelea kufanya kazi yake vizuri, huku ile ya kiungo ikiendelea kucheza kwa uvumilivu katika mazingara yoyote na kutengeneza nafasi, washambuaji watafunga zaidi kwa kuwa ' kikosi chao ni kikubwa' huku kikiwa kimekusanya wachezaji wazoefu ambao wanaweza kushinda katika uwanja wowote, kupata alama 18 kati ya 25 ugenini bila shaka ni mafanikio ambayo hata wewe utahitaji kuona mwisho wa timu hiyo katika ligi kuu.

0714 08 43 08



Comments