Na. Richard Bakana, Dar es Salaam
Mabao ya Simon Msuva pamoja na Amis Tambwe katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, yameiwezesha Yanga SC kurejea kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania bara kwa kufikisha alama 35 mbele ya Azam FC.
Yanga imefanikiwa kurejea katika nafasi yake ya kwanza baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar ambapo kunako dakika ya 7 Msuva aliipachika bao la kwanza kwa mkwaju wa penati.
Iliwachukua dakika 7 tena Yanga wakaongeza bao la pili kunako dakika ya 14 kupitia kwa Amis Tambwe akimaliziakazi nzuri Mrisho Ngassa.
Wakiwa hawajakata tamaa, Wanankurukumbi hao (Kagera Sugar) walijipatia bao la kusawazisha katika dakika ya 39 kwa mkwaju wa penati ambayo ilichongwa na Salum kanoni.
Katika mtanange huo ambao ulikuwa ukichezeswa na muamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani, Kagera Sugar kunako kipindi cha pili walionyesha kusaka bao la kusawazisha na pengine kuongeza bao lakini bahati haikawa yao.
Hussein Javu wa Yanga aliikosesha timu yake bao baada ya kupiga shuti kali ambalo liligonga mwamba wa juu na kutoka nje katika dakika ya 54.
Kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi, Kocha Hans Van De Pluijm aliamua kumpumzisha Mshambuliaji wake Khap Sherman dakika ya 75 na nafasi yake kuchukuliwa na Jerry Tegete ambaye pia hakuonyesha mabadiriko yoyote.
Kufatia Ushindi huo wa Pointi tatu, Yanga inakuwa imejiweka katika kilele cha ligi kwa alama 35 huku ikiwashusha Azam katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 34.
Comments
Post a Comment