Msuva aanguka tuzo ya mwezi



Msuva aanguka tuzo ya mwezi

F

Wambura (kushoto) ameula tuzo ya mchezaji bora wa mwezi

Kiungo wa timu ya Coastal Union, Godfrey Wambura amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Februari 2015 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Wambura amechaguliwa kuwa mchezaji bora baada ya jopo la makocha linalofanya majumuisho ya wachezaji bora wa kila mchezo, ambapo kiungo huyo ameweza kuwapiku wachezaji Saimon Msuva wa Young Africans, Abasirim Chidiebere wa Stand United na  Gideon Benson wa Ndanda FC.

Kwa kuibuka mchezaji bora wa mwezi Februari, Wambura atazawadiwa fedha taslimu sh. milioni moja  kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.

Wakati huo huo timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajiwa kuagwa mbele ya waandishi wa habari kesho alhamisi saa 5 kamili katika ukumbi wa TFF Karume.



Comments