MARIJANI RAJABU, NANI ANAFAIDI HAKIMILIKI ZAKE?



MARIJANI RAJABU, NANI ANAFAIDI HAKIMILIKI ZAKE?
safari trippers

Marijani Rajabu, wa pili toka kulia waliosimama. Hapa likiwa kundi zima la Safari Trippers. Mwenye miwani ni David Mussa kiongozi wa bendi na wa kwanza toka kulia waliosimama ni Jumanne Mwinymvua Uvuruge, mtunzi wa wimbo Georgina

Marijani Rajabu alizaliwa tarehe 03 March, 1955 katika eneo la Kariakoo Dar es Salaam. Siku ya tarehe 23 March 1995 Marijani Rajabu- Jabali la Muziki, Doza aliaga dunia. Tunatimiza miaa 20 toka tulipoonana mara ya mwisho na mwamba huu. Nakumbuka nilipokutana nae mara ya mwisho, alikuwa kiuza kanda za nyimbo zake katika kaduka kadogo alikofungua nyumbani kwake. Alikuwa ana masikitiko kuwa nyimbo zake zilikuwa zikiuzwa mtaa wa pili tu toka kwake na matajiri wakubwa bila ruksa yake na bila yeye kupata chochote na wakati huo afya yake haikuwa nzuri hivyo hata kazi yake ya muziki ilikuwa ngumu kufanya tena. Hata baada ya kifo chake nakumbuka kukutana na mama yake akiwa natafuta njia ya kulipwa na radio zilizokuwa zikipiga nyimbo za mwanae wakati familia ikiwa haipati chcochote. Ni miaka 20 sasa hali haina tofauti yoyote, ni nani asiyejua kuwa karibu kila kata utakuta kanda na CD za nyimbo za Marijani zikiuzwa? Lakini familia yake ikikosa hata senti tano kutokana na mamilioni ya shilingi zinazopatikana kutokana na kazi za Jabali hili. Sheria ya Hakimiliki nchini inampa mtunzi haki za kazi zake kwa maisha yake yote na miaka 50 baada ya kifo chake. Ni wazi kuwa sheria inaagiza kuwa mpaka wakati huu familia ya Jabali ilitakiwa kuwa na mafao kutokana na kazi nyingi za Marijani, lakini bahati mbaya hali si hii. Kuna mafunzo makubwa katika hili kwa wanamuziki ambao kwa wakati huu wako juu ambao hawatumii umaarufu wao kuhamasisha kufwatwa kwa sheria ya Hakimiliki, bahati mbaya ni wasanii wachache sana duniani hubaki maarufu maisha yote hivyo kuweko kwa sheria za haki miliki humuwezesha msanii aendelee kufaidi matunda ya kazi zake hata pale ambapo umaarufu wake umepotea.

Pamoja na muziki Marijani pia alikuwa golikipa mzuri sana, kuna hadithi kuwa katika miaka ya 70 viongozi wa klabu kubwa ya Simba waliwahi kumfuata Marijani wakitaka awe kipa wa timu hiyo, bahati nzuri kwa muziki hilo halikutokea.

Akiwa bado mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Tambaza, Marijani alijiunga na bendi ya shirika la State Trading Corporation (STC). Bendi hiyo ambayo awali ilikuwa ikiitwa The Jets ilipochukuliwa na shirika hilo ikaitwa STC Jazz Band, ilikuwa chini ya Raphael Sabuni, ikiwa na wanamuziki kama Huluka, Belino, Ally Rehani, ilikuwa maarufu kwa kupiga nyimbo mchanganyiko zilizopendwa na vijana wakati ule. Nakumbuka bendi hii ilipotembelea Iringa mwaka 1972wakati huo nikiwa nami sekondari na tayari ni mpiga gitaa, haraka niliwatafuta walikuwa wamefikia katika Lodge iliyoitwa Kilimanjaro Lodge mahala ambapo kwa sasa kuna pub inaitwa 255, nilipomuona Marijani kwa mara ya kwanza akiwa kijana mwembamba mcheshi, na na kumbuka kitu kimoja vizuri, wanamuziki walizunguka mjini na kuweza kununua santuri ya Vox Afrika, bendi moja ya Kongo iliyokuwa chini ya muimbaji Bombenga. Alikuwa akiimba vizuri sana wimbo ulikuwa unaitwa Magui. Baada ya kuupiga mara kadhaa katika record player, Marijani aliuliza wenzie, 'Hivi hapa Tanzania atakuja kuweko muimbaji aimbe vizuri kama huyu?' Hakika nikiusikilliza leo wimbo ule, ni wazi Marijani alikuja kuwa muimbaji bora mno kuliko aliyeimba Magui.

Kupitia bendi ya STC ndipo Marijani kwa mara ya kwanza aliweza kwenda Nairobi ili kurekodi nyimbo kadhaa za bendi hiyo. Wakati huo bendi ikitaka kutoa santuri ilikuwa lazima iende Kenya. Pamoja na wimbo wa kusifu STC uliojulikana kama STC iko hapa Marijani mwenyewe alitunga na kuimba wimbo wa Shida na Ewe ndugu yangu. Baada ya kurudi toka huko uongozi wa shule ya Tambaza uliilalamikia STC kwa kitendo cha kuchukua mwanafunzi na kuzunguka nae akipiga muziki, kwa vile STC lilikuwa shirika la umma Marijani ilibidi aachishwe bendi. Na ndipo mwaka 1972 alipojiunga na Safari Trippers, bendi ya vijana wenzie ambayo ilikuwa ilikuwa chini ya mwanamuziki aliyekuwa na uwezo wa kupiga vyombo kadhaa ikiwemo gitaa na saxophone, David Musa, na hakika hapa ndipo ilikuwa chuo cha kumkuza kiuimbaji na ndipo nyimbo zake nyingi huwa tunazikia siku hizi, kama Georgina, Josephina, Mkuki moyoni na nyimbo nyingi sana katika mtindo wa Sokomoko. Mwaka 1978, Marijani na wanamuziki kadhaa waliihama kutoka Safari Trppers na kuungana na magwiji kutoka bendi nyingine na kuunda bendi ya Dar es Salaam International. Kazi yake huko inajulikana na kibao chake cha kwanza huko kilikuwa Zuwena, na vikafuatia vibao vingi sana. Mwaka huohuo kundi kubwa na Dar International lilihama na kwenda kuanzisha Mlimani Park Orchestra, bahati nzuri au mbaya wakati huo Marijani alikuwa kasimamishwa bendi, hivyo mwenye bendi akamrudisha Marijani kundini kuja kufufua bendi na ndipo tukapata Dar International iliyodumu mpaka vombo vilipokufa miaka ya mwishoni ya 80. Mwaka 1990 Marijana alirudi tena katika ulingo wa muziki akiwa na kundi lililoitwa Afri Culture akiwa na mtindo wa Mahepe ngoma ya wajanja. Bendi hiyo haikuishi sana ikapotea hewani.

Marijani alifariki Alhamisi March 23 1995 katika hospitali ya Muhimbili na kuzikwa 24 March 1995 katika makaburi ya Kisutu.

 

MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YAKE PEMA PEPONI AMINA

 



Comments