Malinzi awaonya Yanga SC kwa Wazimbabwe




Malinzi awaonya Yanga SC kwa Wazimbabwe

bdfNa Bertha Lumala, Dar es Salaam
Wakati kikosi cha Yanga SC kinatarajiwa kuondoka nchini keshokutwa kwenda Zimbabwe kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya FC Platinum, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ameitaka klabu hiyo ya Jangwani kutobweteka na matokeo mazuri ya nyumbani itakapoikabili timu hiyo Jumamosi.

Yanga SC ilishinda mabao 5-1 nyumbani, lakini Malinzi anaamini kazi bado ni nzito kwa mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara kuing'oa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Malinzi amewaambia waandishi wa habari jijini hapa leo kuwa amezungumza na baadhi ya nyota wa Yanga SC na kuwaeleza ukweli kwamba FC Platinum inaweza kufanya kweli Jumamosi na kuwang'oa wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya kimataifa mwaka huu.

Timu za Polisi Zanzibar, Azam FC na KMKM zilitolewa hatua ya kwanza ya michuano ya Afrika mwaka huu na kuiacha Yanga SC upwekeni katika uwakilishi wa nchi.

"Nimezungumza na Nahodha wa Yanga, (Nadir Haroub) Cannavaro pamoja na (Oscar) Joshua, nimewaambia wapeleke ujumbe kwa wachezaji wenzao kwamba Platinum inaweza kubadilisha matokeo nyumbani na kuing'oa Yanga katika mashindano," Malinzi amesema.

"Wanatakiwa kutobweteka, wakapambane kuhakikisha wanapata bao la mapema ugenini ili kuwavunja moyo wapinzani wao."

Endapo Yanga SC ikifanikiwa kuwang'oa Wazimbabwe hao, itakutana na mshindi kati ya Benfica de Luanda FC ya Angola na Etoile du Sahel ya Tunisia katika hatua inayofuata ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika katika ngazi ya klabu.

Etoile iliyomnunua kiungo mshambuliaji wa Simba SC kutoka Uganda, Emmanuel Okwi kwa mali kauli ya dola za Marekani 300,000 misimu miwili iliyopita, ilishinda 1-0 nyumbani mjini Tunis katika mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita.



Comments