Kwa waraka huu TFF imeyumba



Kwa waraka huu TFF imeyumba
malinzi mkutano mkuuMWANZONI mwa wiki iliyopita, niliona moja ya nyaraka za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliokuwa ukisambazwa kwa klabu zab Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Waraka huo ulioitwa "WARAKA VPL 20150314″ ulitolewa Machi 14, mwaka huu na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine kwenda kwa makatibu wakuu wa klabu za VPL ukiwa na kichwa cha habari "Mabadiliko ya Kanuni na Uundwaji wa Kamati ya Kuratibu Mwenendo wa Ligi".

Waraka huo ulisomeka: "Kamati ya Utendaji ya TFF ilikaa 08 Februari 2015, na mojawapo wa ajenda ilikuwa kuangalia mwenendo wa Ligi Kuu na ligi za chini yake. Kikao kiliunda Kamati ya Dharura ya kushughulikia mwenendo wa ligi ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi na uamuzi kwa mujibu wa kanuni jambo lolote lisilo la kawaida, la hatari au lisilo la kiuanamichezo lililotokea katika mchezo wa Ligi Kuu au katika mwenendo wa shughuli za Ligi Kuu."

Waraka huo pia ulieleza kuwa Kamati ya Utendaji ilifanya mabadiliko katika Kanuni ya Na. 37 na sasa timu itaruhusiwa kuomba kuahirishwa adhabu ya kadi tatu za njano. Kanuni hiyo ya 37(3) sasa inasomeka:

"Mchezaji atayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu, ataruhusiwa kuchagua mchezo mmoja atakaokosa kwa klabu yake kuandika barua kwa chombo kinachoendesha ligi na kuutaja mchezo atakaokosa. Uchaguzi ni ndani ya mechi tatu zijazo, na iwapo itakuwa imebaki mechi moja ligi kumalizika, hakutakuwa ba fursa ya kuchagua."

"Kwa mujibu wa Ibara ya 36(7) cha Katiba ya TFF, uamuzi unaofanywa na vikao vya Kamati ya Utendaji, utekelezaji wake unaanza mara tu baada ya kikao husika kumalizika. Tunaomba samahani kwa usumbufu uliosababishwa na kuchelewa kwa waraka huu," ulifafanua zaidi waraka huo.

Wiki mbili zilizopita gazeti hili lilielezwa kwa kina kuhusu udhaifu wa mabadiliko yaliyofanyika katika kanuni husika, sababu kubwa ikiwa ni kutowiana na kanuni za mashindano za mashirikisho ya soka ya kimataifa kuanzia CECAFA, CAF hadi FIFA.

Lakini, kutolewa kwa waraka huo kunatoa ishara mbaya ya kuyumba kwa uendeshwaji wa TFF kunakokwenda sanjari na kuonekana kama kuna kubebwa kwa baadhi ya klabu na shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini.

Kama ilivyodokezwa hapo awali, waraka wa mabaliko ya Ibara ya 37(3) cha Kanuni za Ligi za TFF ulitolewa Machi 14 mwaka huu, lakini klabu ya Simba ilikuwa tayari imeshaanza kutumia kanuni mpya ilhali ilikuwa haijasambazwa kwa klabu.

Ikitumia kanuni mpya ambayo ilikuwa haijazifikia klabu, Simba iliandika barua kuiomba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuwaruhusu wachezaji wake wawili Abdi Banda na Ibrahim Ajibu kucheza mechi za VPL dhidi ya Stand United, Tanzania Prisons na Yanga ilhali walikuwa na kadi tatu za njano kila mmoja.ajibu na mpira
Banda aliombewa ruhusa kucheza dhidi ya Stand usukumani mjini Shinyanga Februari 22 ilhali alikuwa na kadi tatu za njano huku Ajibu akicheza mechi dhidi ya Prisons Februari 28 na Yanga Machi 8 ilhali alikuwa na kadi tatu za njano (alicheza dhidi ya Yanga akiwa na kadi nne za njano).

Je, Simba ilipataje kanuni mpya na kuanza kuitumia ilhali waraka wa mabadiliko ya kanuni ulikuwa haujasambazwa kwa klabu na TFF?

Viongozi wa Yanga kwa nyakati tofauti wiki mbili zilizopita walikaririwa wakidai kuwa ushiriki wa Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' katika vikao vya Kamati ya Utendaji ya TFF ndiyo unaoifanya klabu hiyo ya Msimbazi kupata nyaraka za TFF kabla ya kuzifikia klabu nyingine. Kaburu ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.

Si lengo langu kuchambua utendaji wa TFF, lakini kumeonekana kama misingi ya kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia miiko haikufuatwa katika utekelezaji wa maazimio ya kikao cha Februari 8 cha Kamati ya Utendaji ya shirikisho.

Shime, TFF irudi katika misingi ya weledi maana mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo. Waraka huu unalidhalilisha shirikisho.

Uchambuzi huu umeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi wa michezo mwandamizi wa gazeti la Nipashe.

CHANZO: NIPASHE



Comments