Na. Richard Bakana, Dar es Salaam
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Mpira wa Ufukweni Maarufu kama Beach Soccer, John Mwansasu amesema kuwa anatambua uwezo wa Misri, lakini kama mwalimu wa Timu amewaandaa wachezaji wake kupambana hapo siku ya Ijumaa wiki hii ili kupata ushindi na kujiweka sehemu nzuri ya kutinga katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mchezo huo.
Akizungumza na Shaffihdauda.com Mwansasu amesema kuwa licha ya ukubwa wa jina la Misri katika Soccer lakini yeye anaamini katika kujituma na nidhamu kubwa ya mchezo.
"Tunaelewa kuwa ni timu ambayo imeendelea sana, Wenzetu wameanza muda mrefu sio katika Beach Soccer tu, Mimi pamoja na timu tunaamini katika kujituma, Kama unavyojua tunawachezaji ambao wanavipaji vya hari ya juu na kwenye mchezo huu unajua tunacheza wanne kwa wane, Kwahiyo unapocheza na timu ambayo ipo juu lazima ucheze kwa nidhamu, Tumewajenga wachezaji kuwa na nidhamu ya ukabaji, Misri tunawaheshimu ni timu nzuri kwahiyo na sisi lazima tucheze kwa nidhamu" Amesema Mwansasu.
Akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo huo, Kocha huyo ambaye aliiongoza Timu hiyo kuiondo Kenya katika michuano hiyo, amesema kuwa leo wamefanya mazoezi asubuhi, Lakini jana wachezaji wote walikuwa wakifanyiwa matibabu na Daktari wa Timu kufatia baadhi ya wachezaji kuwa na majeraha kidogo.
"Maandalizi yanaendelea vizuri, jana jioni ilikuwa ni siku ya mapumziko kwa sababu Daktari alikuja kuwapa tiba wachezaji timu nzima kama unavyojua wachezaji Ally Rabby na Samwel John walikuwa wanasumbulia na maumivu ya kigole, Kwahiyo hawa ndio majeruhi tuliokuwa nao na Daktari amesema watakuwa vizuri hadi kufikia Ijumaa" Amesema Kocha Mwansasu.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika michuano ya Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Beach Soccer ambayo imewahi kufanyika mara sita, Misri imewahi kushiriki mara Nnee, Waarabu hao wamefanikiwa kushika nafasi ya nne mara mbili, na Nafasi ya tatu mara mbili. Huku Tanzania ikiwa ndi mara ya kwanza ikisaka nafasi ya kushiriki Fainali hizo na Timu yake ya Taifa ikiwa na Mwaka mmoja toka ianzishwe.
Endapo Kocha John Mwansasu atafanikiwa kuwaondoa Wamisri katika hatua hiyo ya pili basi wataingia moja kwa moja katika fainali za Kombe la Afrika zitakazo fanyika nchini Visiwa vya Shelisheli mwezi huu.
Comments
Post a Comment