Alhamisi iliyopita mkurugenzi wa Mashauzi Classic, Isha Ramadhani maarufu kama Isha Mashauzi, aliunguruma kwenye studio za Radio Uhuru jijini Dar es Salaam na kufafanua mambo kadhaa juu ya malengo yake ya mwaka 2015.
Isha akazungumzia juu mpango wake wa kutengeneza nyimbo nje ya taarab huku tayari akiwa ameshaachia vibao viwili "Nimlamu Nani" na "Nimpe Nani" ambavyo vipo katika miondoko ya rumba na zouk.
Mwimbaji huyo mwenye sauti tamu akasema ameamua kufanya mradi nje ya taarab ili kupanua wigo wa mashabiki.
Isha alisema: "Wako mashabiki wengi ambao wananipenda mimi kama Isha lakini si wapenzi wa taarab, nikaona si vibaya nikawafikiria na wao na kuwapa kitu roho inapenda.
"Kwa kufanya hivyo najua itasaidia kuwavuta watu hao kwenye maonyesho ya bendi yangu na kuzidi kuboresha pato letu.
"Lakini kwa kufanya hivyo pia nakuwa nimetoa fursa ya kuwafanya watu wafahamu uwezo wangu wa uimbaji, ninaweza kuimba aina yoyote ya muziki kuanzia taarab, dansi, bongo fleva, mchiriku na hata reggae, hivyo ndivyo mwimbaji bora anavyopaswa kuwa."
Katika mahojiano hayo yaliyorushwa kupitia kipindi cha "Tashtiti Zetu" Isha ambaye pia aligusia mambo mengine mengi ikiwemo namna ya kuwanyanyua wasanii chipukizi, alikuwa akihojiwa na watangazaji Nuru Suleiman na MC Jojoo Tanzania
Kipindi cha "Tashititi Zetu" husikika Jumatatu hadi Ijumaa saa 6 mchana mpaka saa 8 za mchana.
Saluti5 katika pekua pekua yake ikagundua kuwa mbali na Isha kuachia nyimbo mbili, lakini tayari ana nyimbo nyingine tatu ambazo zimeshakamilika ukiwemo mmoja wa mchiriku uliopewa jina la "Ado Ado".
Comments
Post a Comment