Na Augustino Mabalwe,Dar es salaam
Baada ya kukaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha, hatimaye kiungo mshambuliaji wa klabu ya Real Madrid James Rodriguez arejea mazoezini kufuatia matibabu mazuri aliyopatiwa na madaktari wa timu hiyo.
Rodriguez,23, alivunjika mfupa wa ndani katika mguu wake wa kulia mapema mwezi Februari katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Sevilla.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na matajiri hao msimu huu kwa ada ya paundi milioni 63 kutoka Monaco mpaka anapata majeraha hayo tayari alishaifungia klabu hiyo magoli 7 na kutoa pasi za mwisho 7 katika mechi 22 alizocheza kwenye michuano yote msimu huu.
Mshindi huyo wa tuzo ya goli bora (Puskas) la mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014 amekosa mechi nyingi kipindi akiuguza majeraha yake na sasa amesema amerejea kwa kasi kuisaidia timu yake.
Aidha kuelekea mechi za robo fainali klabu bingwa dhidi ya Atletico Madrid mwezi ujao hii ni habari nzuri kwa kocha wa klabu hiyo Carlo Ancelotti ambaye amekuwa akimtumia mcolombia huyo katika nafasi tofauti ndani ya uwanja.
Comments
Post a Comment