Cannavaro wa Stars si huyu wa Yanga


Cannavaro wa Stars si huyu wa Yanga

canavaro yangaUKITAKA kutaja orodha ya mabeki 10 bora wa kati katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, bila shaka hutamsahau Nadir Haroub 'Cannavaro', beki wa kati ya Yanga.

Mzaliwa huyo wa Zanzibar ni miongoni mwa wachezaji wachache waliokaa kwa muda mrefu katika kikosi cha wanajangwani.

Amekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha safu ya ulinzi, kuwaongoza wachezaji wengine na kufunga mabao muhimu.

Nahodha huyo wa Yanga na Taifa Stars ni miongoni mwa wachezaji wachache nchini wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya vichwa.

Miongoni mwa mabao yake bora ya vichwa ni lile lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya Al-Ahly katika mechi ya kwanza ya hatia ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwaka jana na lile lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union katika mechi yao ya VPL msimu huu.
Hata hivyo, katika siku za karibuni mwenendo wa Cannavaro umekuwa si mzuri ndani ya kikosi cha Mholanzi Hans van der Pluijm cha Yanga tofauti na anapokuwa kwenye kikosi cha Mholanzi Mart Nooij cha Taifa Stars.nooj

Ikumbukwe kuwa Cannavaro amesota kwa muda mrefu kurejeshwa Taifa Stars hadi msimu uliopita alipong'ara na Yanga VPL na katika michuano ya kimataifa.

"Al Ahly wamenisaidia kuitwa tena Taifa Stars, nimefanya vizuri katika mechi za kimataifa kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu wa Yanga," alikaririwa Cannavaro baada ya kuitwa tena Stars msimu uliopita.

Kwa wanaofuatilia kwa kina soka la Tanzania, watakubaliana na mimi kwamba katika siku za karibuni mwenendo wa Cannavaro kitabia akiwa na kikosi Stars ni mzuri kuliko anavyokuwa katika kikosi cha Yanga.

Tangu kuanza kwa msimu huu wachezaji watatu wa Yanga wametolewa uwanjani na marefa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu. Wachezaji hao ni Cannavaro, Danny Mrwanda na Haruna Niyonzima 'Fabregas'.

Cannavaro ndiye beki pekee wa Yanga aliyekumbwa na adhabu hiyo alipocheza rafu mbaya na kuigharimu timu yake kulala 1-0 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Novemba Mosi, mwaka jana.

Mrwanda alitolewa kwa kadi ya pili ya njano na kuigharimu Yanga kulala 2-1 ugenini dhidi ya BDF XI FC katika mechi yao ya marudiano ya hatua ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwenye Uwanja wa SSKB Lobtse, Botswana mwezi uliopita.

Niyonzima pia alitolewa kwa kadi ya pili njano katika mechi yaliyolala 1-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba katika mechi yao ya mzunguko wa pili wa VPL kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 8.

Mbali na kadi nyekundu iliyokifanya kikosi cha Yanga kikosi huduma katika mechi tatu za VPL msimu huu, Cannavaro ameendelea kufanya vitendo vinavyoashiria utovu wa nidhamu uwanjani akiwa na kikosi cha Yanga.

Dakika mbili baada ya kuanza kwa kipindi cha pili cha mechi yao waliyoshinda 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa, Cannavaro alifanya kitendo kinachoashiria utovu wa nidhamu alipolipa kisasi dhidi ya Fully Maganga.

Katika purukushani na kuwania mpira ndani ya boksi la Yanga, Mganga alimsukuma Cannavaro, ambaye licha ya kipenga kupulizwa, aliinuka na kumpiga kwa kifua mshambuliaji huyo na kumdondosha.

Cha kushangaza refa Simon Mberwa alimuonya kwa kadi ya njano Mganga na refa huyo kutoka Pwani hakuchukua hatua zozote dhidi ya Cannavaro, kinyume cha Sheria Na. 12 ya Soka (Faulo na Tabia Mbaya).

Kosa alilolifanya Cannavaro halipishani na kosa lililomgharimu Zinedine Zidane wa Ufaransa alipotolewa kwa kadi nyekundu kutokana na kumpiga kichwa kifuani Marco Materazzi wa Italia, tena pasipo na mpira katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2006.

Tukio baya zaidi linalomhusu Cannavaro uwanjani msimu huu ni pale alipomkumbatia na kumpiga mabusu askari polisi mwanamke katika mechi ya VPL ambayo Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa Februari 4.

Baada ya kufunga bao pekee la mchezo akimalizia kwa kichwa mpira wa kurushwa kama kona wa mchezaji 'kiraka' wa Yanga, Mbuyu Twite dakika ya 11 ya mchezo, Cannavaro alikwenda kando ya uzio mdogo wa ndani ya Uwanja wa Mkwakwani na kufanya udhalilishaji huo dhidi ya askari huyo aliyekuwa kazini na sare za Jeshi la Polisi.

"Cannavaro ni mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu anapokuwa Taifa Stars, lakini tabia zake akiwa na kikosi cha Yanga zimekuwa mbaya. Ninafikiri ni kwa sababu katika safu anayocheza Yanga anapangwa na watu ambao baadhi yao tabia zao si nzuri. Huenda ameanza kuziiga," alisema mmoja wa wachambuzi wa kituo cha Azam TV katika mahoajino na NIPASHE jijini hapa mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Mgambo.

Binafsi ninafikiri ipo haja benchi la ufundi la Yanga linaloongozwa na Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa, kukaa na Cannavaro na kumweleza ukweli kuhusu mwenendo wake kitabia siku hizi maana usipoziba ufa, utajenga ukuta.

Cannavaro wa Yanga wa sasa si Cannavaro wa Taifa Stars. Cannavaro wa Jangwani wa sasa si mfano mzuri kwa watoto na ustawi wa soka la Tanzania ikizingatiwa yeye ni nahodha wa timu kubwa ya Yanga na Taifa Stars.

Uchambuzi huu umeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi wa michezo mwandamizi wa gazeti la Nipashe.

CHANZO: NIPASHE



Comments