30 Yanga SC kuifuata Platinum Jumatano


30 Yanga SC kuifuata Platinum Jumatano

yanga jjjjNa Bertha Lumala, Dar es Salaam
Msafara wa watu 30 wa Yanga SC, wakiwamo viongozi, utaondoka jijini hapa Jumatano kwenda Zimbabwe kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Platinum FC, mtandao huu umeelezwa.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, katika mahojiano na mtandao huu jijini hapa muda mfupi uliopita, amesema kikosi chao kilichopiga kambi jijini hapa, kitasafiri kuwafuata wapinzani hao Aprili Mosi, yaani Jumatano.

Amesema kila kitu kimekamilika kwa ajili ya safari hiyo na wana uhakika wa kufanya vyema na kuwang'oa wapinzani wao hao.

"Wachezaji waliokuwa na timu zao za taifa, wataanza kuingia kambini leo jioni. Mashabiki wetu wataondoka Jumanne. Maandalizi yote yamekamilika, kila kitu kiko safi na tumejipanga vyema kwa ajili ya mechi," amesema Muro.

Yanga SC ilitanguliza mguu mmoja kusonga katika hatua ya pili ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya timu hiyo iliyoing'oa Sofapaka FC ya Kenya katika hatua ya awali.

Endapo Yanga SC  ikifanikiwa kuwang'oa Wazimbabwse hao, itakutana na mshindi kati ya Benfica FC ya Angola na Etoile du Sahel ya Tunisia katika hatua inayofuata ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika katika ngazi ya klabu.

Benfica FC na Etoile du Sahel FC iliyomnunua Emmanuel Okwi wa Simba SC misimu miwili iliyopita, ni miongoni mwa timu tajiri barani Afrika na zimekuwa zikisajiri wachezaji 'mafundi' na wenye uwezo mkubwa.

Etoile du Sahel FC ilishinda 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Tunis, Tunisia wiki mbili zilizopita.



Comments