VPL: Simba kufia uwanjani, Mbeya City nao majaribuni!



VPL: Simba kufia uwanjani, Mbeya City nao majaribuni!

s10

WEKUNDU wa Msimbazi Simba kesho wanaikaribisha Tanzania Prisons katika mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara itayopigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam majira ya saa 10:00 jioni.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mnyama alivutwa sharubu kwa kufungwa goli 1-0 na Stand United uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga wakati Prisons walitoka suluhu (0-0) na Azam fc uwanja wa Azam Complex.

Mechi ya kwanza mjini Mbeya, timu hizi mbili zilitoka sare ya 1-1.

Timu zote zitaingia kusaka ushindi ili kuendelea kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi kuu, hususani Prisons wanaoburuza mkia kwa kujikusanyia pointi 12 tu katika mechi 15 walizocheza.

Simba wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 20 kibindoni na hata kama watashinda kesho wataendelea kuwa nyuma ya Kagera Sugar wenye pointi 24 nafasi ya tatu na Wakata miwa hao kesho watacheza na Stand United,  Kambarage.

Kagera wafungwe wasifungwe, wataendelea kukaa katika nafasi yao.

Mechi nyingine ya kukata na shoka itazikutanisha klabu za Mbeya City na Ruvu Shootings uwanja wa CCM Sokoine, Mbeya.

City waliojeruhiwa 3-1 na Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita wataingia uwanjani kusaka pointi tatu muhimu ili kurudisha imani kwa mashabiki wake.

Klabu hiyo inayonolewa na kocha bora wa msimu uliopita, Juma Mwambusi inashika nafasi ya 12 kwa kujikusanyia pointi 17 katika mechi 15 ilizocheza.

Mechi nyingine itapigwa dimba la CCM Mkwakwani Tanga ambapo Mgambo JKT wataikaribisha Coastal Union.



Comments