Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Niliuponda sana usajili wa Simba SC wakati wa majira ya usajili katikati ya mwaka uliopita, nilikosoa namna ' kamati ya usajili' chini ya Zacharia Hans Poppe ilivyokuwa inafanya kazi yake ' kiholela', Poppe kama mkuu wa kamati hiyo alishindwa kabisa kutekeleza mahitaji ya mwalimu Z.Logarusic ambaye alipendekeza wachezaji kadhaa kutemwa na wengine kusajili. Nakumbuka, LOGA alipendekeza majina ya wachezaji 15 wa kuachwa huku akisema kuwa 'hawana hadhi ya kuichezea klabu hiyo kubwa na yenye histori ya kuvutia' Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Edward Christopher, Henry Joseph, Zahoro Pazzi, Mkenya, Donald Mosoti, Mrundi, Gilbert Kaze, ni baadhi ya wachezaji waliondoka klabuni hapo kwa sababu tofauti, kumalizika kwa mikataba, kushuka kwa viwango na mambo ya kinadhamu yalichangia kuwaondoa mastaa ili kupisha ujenzi wa timu hiyo katika timu hiyo ambayo inasotea nafasi mbili za juu katika ligi kuu Bara kwa msimu wa tatu sasa.
" Usajili uliofanywa haukuwa mzuri, sasa wanavuna matokeo ya usajili ambao haukukidhi mahitaji ya klabu kubwa kama Simba" anasema kiungo mshambulizi wa zamani wa timu hiyo, Ulimboka Mwakinge ambaye alifunga magoli matatu katika hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka, 2003.
ULI, mchezaji aliyekuwa na kasi, nguvu, chenga na maarifa binafsi awapo uwanjani anaweza kuonekana ni mnafiki kwa maneno yake hayo lakini ndiyo ukweli ulivyo. Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni kama amefikisha ujumbe mzito kwa klabu hiyo kuachana na kamati zake za usajili na kuwatumia ' ma-scout' kama sehemu sahihi kuwatafuta wachezaji sahihi ambao wataendana ki-mfumo na ki-utamaduni wa kiuchezaji wa klabu.
" Tatizo la Simba hivi lilianzia katika usajili, kwa maana kwamba walisajiliwa wachezaji wasio na hadhi ya kuichezea timu hiyo". Simba imekuwa na matokeo yasiyoridhisha msimu huu kwani wameshinda mara nne tu katika michezo 15 waliyocheza. Ikiwa tayari imepoteza michezo mitatu na kutoa sare mara nane mabingwa hao mara 19 wa kihistoria wa Bara wamezidiwa alama 11 na timu iliyo kileleni. Yanga SC, vinara wa ligi hiyo tayari wamepoteza michezo miwili msimu huu, yote katika viwanja vya ugenini.
Kagera Sugar ambayo iliifunga Yanga mjini Bukoba ilikuwa timu ya kwanza kuifunga Simba katika uwanja wa Taifa, Dar bs Salaam msimu huuh kisha Mbeya City ikafuatia. Baada ya kipigo cha tatu katika msimu na cha kwanza ugenini msimu huu kutoka kwa Stand United wiki iliyopita, Simba ni kama haina uwezo wa kushinda ubingwa ambao waliupata kwa mara ya mwisho msimu wa 2011/12 kwa kuwa wamekuwa na matokeo mabaya zaidi katika uwanja wa nyumbani huku wakiwa hawana uhakika wa kupata ushindi katika viwanja vya ugenini.
Comments
Post a Comment