Tanzania yaifumua Kenya 7-6 Beach Soccer, sasa kuwawinda Misri


Tanzania yaifumua Kenya 7-6 Beach Soccer, sasa kuwawinda Misri

beach soccer leWachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ya Beach Soccer wakiwa mazoezini na Kocha wao John Mwansasu.

Na. Richard Bakana, Dar Es Salaam

Timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa ufukweni (Beach Soccer) leo imefanikiwa kuiondoa Kenya katika mbio za kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa mchezo huo baada ya kuifunga kwa mabao 7-6.

Akizungumza na Shaffihdauda.com baada ya Mchezo ambao umepigwa jioni hii katika fukwe za Escape One Jijini Dar es salaam. Meneja wa Timu hiyo, Deo Lucas, amesema kuwa siri ya ushindi huo ni maandalizi  mazuri kabla ya kukutana na Kenya, ambao walikutana nao wiki jana katika mji wa Mombasa na Tanzania ikiwa ugenini ikaibuka na ushindi wa jumla ya mabao 5-3.

Deo amesema kuwa wapinzani wao Kenya walikuwa wazuri zaidi tofauti na mchezo wa kwanza walipokutana kitu ambacho kilifanya mchezo kuwa mgumu sana kwao licha ya kupata ushindi mnono.

"Mchezo ulikuwa mzuri ila mgumu, Kenya walikuwa wazuri sana na walikuwa wamejipanga lakini Tulijiandaa vizuri, Watanzania inatakiwa watupe nguvu kwa kujitokeza na kutushangilia sana tunapocheza" Amesema Deo Lucas Meneja wa Timu ya taifa ya Beach Soccer.

Kutokana na Ushindi huo Tanzania inakuwa imesonga mbele kwa jumla ya mabao 12 kwa 9 ,Mwezi Machi kikosi hicho kitasafiri hadi nchini Misri kucheza nao mchezo wa awali kabla ya kurudiana baada ya wiki moja.

Endapo Tanzania itafanikiwa kuwafunga na kuwaondoa Misri basi moja kwa moja itakuwa imetinga katika fainali za Mataifa ya Afrika ambayo kilele chake itakuwa mwezi Aprili mwaka huu nchini Shelisheli (Visiwani).

"Jumatatu wachezaji wataenda mapumziko kwa siku nne na kurejea Kambini tayari kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri, " Amesema Deo.

Pongezi za Dhati kwa kapteni wa Tanzania Beach Soccer, Ally Rabbi ambaye alifunga mabao manne pekee na kuipa timu yake ushindi huo mnono.



Comments