Prisons walia na TFF kipigo cha Yanga (3-0)


Prisons walia na TFF kipigo cha Yanga (3-0)

mwamaja PrisonsKocha wa Tanzania Prisons, David Mwamaja, akiongea na waandishi wa habari.

Na. Richard Bakana. Dar es salaam

Kocha mkuu wa Tanzania Prisons David Mwamaja, ameonyesha kutoridhishwa na matokeo dhidi ya Yanga katika mtanange uliopigwa kunako Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya na kupoteza kwa jumla  ya mabao 3-0, ambapo  zigo la lawama amelielekezea kwa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzanaia.

Akizungumza na Shaffihdauda.com baada ya mchezo wa jana dhidi ya Azam, Mwamaja amesema kuwa kitendo cha kusafiri kwa basi kutoka Mbeya hadi Dar es salaam kujiandaa na mechi ya Azam hapo hapo wakatakiwa kurudi Mbeya kucheza na Yanga SC katikati ya wiki ilikuwa ni kuwadhohofisha wachezaji wao.

Katika kupigania hilo Kocha huyo amesema kuwa walijaribu kuomba uongozi wa TFF japo ujaribu kuwapa tiketi za Ndege lakini ilishindikana kitu ambacho kilipelekea kucheza na Yanga wakiwa wamechoka na kuambulia kipigo hicho.

"Tumepoteza mchezo wa juzi (Dhidi ya Yanga) sababu ya kuzungushwa na chama cha mpira, kwasababu huwezi mtu akaja kutoka Mbeya, kujiandaa na mchezo wa Azam, alafu unambadirisha arudi tena kule ambako anakaa siku moja na kucheza kitu ambacho wachezaji lazima wachoke sana" Amesema Mwamaja ambaye jana amefanikiwa kuibuka na pointi moja baada ya kutoa sare na Azam katika uwanja wa Chamzi kwa 0-0.

"Tulijaribu kulalamika kwamba, iwe mbadara, tupeni ndege turudi nyie simmepanga hivi karibu karibu, lakini mimi naamini tutaenda vizuri ninawaamini wachezaji wangu" Amemalizia David Mwamaja.

Katikati  ya juma lililopita TFF ilitoa ratiba mpya ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara  ambayo imezingatia baadhi ya mechi za viporo, mechi za Kimataifa ambazo huwakirishwa na Yanga katika Kombe la Shirikisho na Azam FC kunako Klabu Bingwa, kitu ambacho kilifanya Tanzania kucheza na Yanga katikati ya juma na kuambulia kipigo hicho cha bao 3-0.

Lakini kocha Mwamaja yeye anaizungumzia ratiba hiyo na kusema hivi "Ratiba yenyewe ipo vizuri lakini ilikuwa tu kwa hiyo juzi, mtu unaweza kusema labda kunakitu watu wanatengeneza" .



Comments