BAADA ya kuwa nje kwa majeruhi muda mrefu, kiungo mshambuliji wa Mbeya City Fc, Alex Seth 'Messi' amerejea kikosini tayari kuendeleza mapambano katika kindumbwendumbwe cha ligi kuu ya soka Tanzania Bara.
Seth amekaririwa na Tovuti ya Mbeya City fc akisema kuwa anamshukuru Mungu kwa kupona majereha yaliyokuwa yanamsumbua kwa kipindi kirefu na kumfanya kuikosa ligi kwa kipindi kirefu.
"Nashukuru nimepona,nilikosa ligi kwa kipindi kirefu mara ya mwisho nilicheza dhidi ya Tanzania Prison msimu uliopita,narudi kuongeza nguvu kwenye kikosi, kama timu tulikuwa na wikiendi mbaya baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Yanga lakini jumamosi hii naimani itakuwa ni sehemu nyingine ya furaha kwetu hasa kwa kuongeza pointi tatu muhimu dhidi ya Ruvu Shooting" alisema.
Akiendelea zaidi Seth alisema, hivi sasa kwenye kikosi imani ya kila mchezaji ni kucheza kwa nguvu ili kutafuta matokeo kwenye mchezo ujao huku akiamini kuwa hilo linawezekana hasa ukizingatia morali iliyopo hivi sasa miongoni mwa nyota wa City bila kujali nini kilikuwepo juma lililopita.
"Naomba mashabiki wawe na timu yao, bado iko vizuri na kwa uwezo wa mwenyezi mungu naimani tutashinda jumamosi, tunajua walikosa furaha baada ya mchezo uliopita lakini huu ni wakati wao na waamini kwenye soka inawezekana kushinda mchezo unaofuata hata kama ulipoteza mchezo uliopita" alimaliza.
Comments
Post a Comment