‘ Manchester City watafurukuta Camp Nou, ila hawana nafasi ya kusonga mbele….’


' Manchester City watafurukuta Camp Nou, ila hawana nafasi ya kusonga mbele….'

260DC29600000578-2967466-image-a-94_1424815556629

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

 Manchester City ni kama wako karibu na ' mlango wa kutokea' katika michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya msimu huu kufuatia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa FC Barcelona usiku wa Jumanne katika dimba la Etihad. Mshambulizi ' mtukutu' na mfungaji bora wa ligi kuu ya England msimu wa 2013/14, Luis Suarez alilipata thamani ya usajili ghali zaidi katika klabu kwa kuifungia timu yake ya Barcelona magoli mawili ' maridhawa'.

 Suarez alifunga goli la kwanza katika dakika ya 16, kisha akafunga lingine robo saa ya pili ya mchezo na mabao hayo yalisimama hadi mwisho wa mchezo licha ya wenyeji kufunga bao pekee kupitia kwa mshambulizi wa zamani wa Atletico Madrid, Sergio Aguero. Bao hilo la Aguero walau linaweza kurudisha matumaini ya City kusonga mbele na kufuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza.

 City ni klabu inayojijenga hivi sasa barani ulaya, ikiwa imeshinda mataji mawili ya ligi kuu England katika misimu minne iliyopita, bila shaka klabu hiyo ya Manchester imeshajiweka katika tawi moja na klabu kubwa nchini humo, namaanisha Manchester United, Liverpool, Chelsea na Arsenal. Ubora wao nchini England umetajwa ni ' matumizi makubwa ya pesa', jambo ambalo halina shaka.

 Baada ya Suarez kufunga goli ' kali', nahodha wa City Vicent Kompany alikuwa ' amepiga magoti' sijui alikuwa akimaanisha nini lakini ilikuwa ni kama kuhitaji ' huruma' wasiendelee kufungwa zaidi. Mshambulizi huyo wa zamani wa Liverpool alikuwa na kasi, huku akionesha ' kiwango kipya' . Baadhi ya mashabiki na waandishi wa habari wa Kimataifa wamesifu mno kiwango cha Mruguay huyo huku wakisisitiza kuwa ' huyu ndiye Suarez ambaye Barca' ilimuhitaji.

 City bado wana uwezo wa ' kujitetea' lakini matuaimi ni madogo nap engine nafikiri wanahitaji misimu mingine miwili hadi mitatu ili kufika walau robo fainali kwa mara ya kwanza katika michuano ya mabingwa ulaya. Matumizi makubwa ya pesa hayawezi kuwa sababu pekee kwa City kuingia miongoni mwa klabu ' vigogo' barani ulaya. City inahitaji subira, inahitaji muda zaidi kupenya miongoni mwa klabu nane bora za ulaya kwa kuwa tayari kuna klabu zimejijenga kimbinu, kiufundi na kiuzoefu.

 Msimu uliopita walipovuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza walikutana na Barca katika hatua ya 16 bora. Barca ambayo ilikuwa haina makali ilishinda katika michezo yote miwili na kufuzu kwa robo fainali kwa jumla ya mabao 4-1. City ilichapwa 2-0 katika uwanja wa nyumbani na kupoteza 2-1 Nou Camp. Ikiwa ni mwaka mmoja sasa umepita, klabu zote zimekuwa na mabadiliko. City imeshuka kiwango, huku Barca ikionekana ' kufufuka upya' na kurudi katika makali yake ya kawaida.

 Inawezekana City ikahitaji kocha mpya zaidi ya Manuel Pellegrini ambaye atakuwa na uwezo wa kuivusha timu hiyo mbele zaidi wakati itakapokuwa ikicheza kwa mara ya tano mfululizo michuano hiyo msimu ujao. Wakati walihitaji nguvu na maarifa zaidi ili kuishinda AS Roma jijini Rome ili kupata nafasi ya kufuzu kama washindi wa pili wa kundi nyuma ya Bayern Munich, City bado timu change nap engine inahitaji mabadiliko makubwa kwa mara nyingine ili kuingia ' top 8' ulaya.

 Kabla ya kuivaa Bayern mwezi Novemba, kiungo wa City, Samir Nasri alisema kuwa endapo wangeshindwa kuifunga Munich na kufuzu kwa hatua ya 16 bora basi wachezaji wengi mastaa wamgeondolewa. Hiyo ilikuwa kauli ngumu kueleweka lakini ni ukweli kuwa klabu hiyo itawaondoa wachezaji wengi mwishoni mwa msimu ili kusuka timu ya ulaya. Ili kutwaa ubingwa wa ulaya ni lazima uzifunge klabu kubwa kama Barca, Real Madrid, Munich, Chelsea n.k, na hauwezi kuzishinda kiurahisi kama uwezo wako utakuwa mdogo kiufundi, kimbinu na kiuzoefu.

 City ni bora ndiyo maana licha ya kucheza pungufu waliweza kufika mara kadhaa katika lango la Barca na kufunga goli ambalo limewafanya kujiandaa na safari ya Camp Nou wiki tatu zijazo wakiwa na ' matumani'. Mara mbili wamekuwa wakipata kadi nyekundu dhidi ya Barca. Msimu uliopita ilikuwa ni mlinzi wa kati, Martin Demichels na msimu huu imetokea kwa mlinzi wa kushoto, Gael Clichy.

 Wote hao wamepata kadi hizo katika uwanja wa Etihad na bahati mbaya wote wanauzoefu mkubwa katika michuano hiyo kwani Martin amewahi kuwa nguzo katika ngome za Bayern Munich na Malaga wakati Clichy alicheza kwa zaidi ya misimu nane akiwa na klabu ya Arsenal. City wanakosa uzoefu wa kitimu na si mchezaji mmoja mmoja barani ulaya hivyo hata kama Pellegrini atakuja kuondolewa kwa kigezo cha kushindwa ulaya nasi mtu atakaye fuata anapaswa kuwa kocha mwenye tabia na hulka  ya Jose Mourinho.

 Kucheza dhidi ya timu kubwa kama Barca si jambo rahisi, huku Barca hiyo ikiwa na Leo Messi, Neymar Jr na Suarez katika safu ya mashambulizi. City wamestahili kufungwa na Barca na wamekuwa na bahati kupata goli dhidi ya mabingwa hao mara nne wa kihistoria ambao sasa wameimarika kimwili na kiakili.

 Mwisho wa City ni Camp Nou msimu huu, na wanahitaji misimu miwili hadi mitatu zaidi ili kufuzu kwa robo fainali ya kwanza Ligi ya mabingwa ulaya. Suarez ambaye ameonekana katika ardhi ya England achana naye, Cataluna watakutana na ' mfalme' Messi, ' mchezaji wa maajabu' Neymar ambao walifichwa na makali ya Luis Suarez pale Etihad.

 0714 08 43 08



Comments