Aliyewaburuza Samatta, Cannavaro, tuzo za mwanamichezo bora, aitwa Twiga Stars kuivaa Zambia


Aliyewaburuza Samatta, Cannavaro, tuzo za mwanamichezo bora, aitwa Twiga Stars kuivaa Zambia

Selder Boniface

Mwanamichezo bora wa 2013/2014 Shelder Boniface, Ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars.


Na. Richard Bakana, Dar es salaam

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars), Rogasian Kaijage, amemuita mwanamichezo bora wa mwaka 2013/2014. Shelder Boniface katika kikosi cha wachezaji thelathini (30) kitakachoingia kambini siku ya jumapili (Feb 22)kujiandaa na mchezo wa kufuzu Mataifa ya Afrika dhidi ya Zambia mwezi Machi mwaka huu.

 

Shelder aliibuka mshindi wa Tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka katika usiku wa tuzo zilizofanyika Desemba 12. 2014, ndani ya ukumbi wa VIP Diamondi Jubilee na kushuhudiwa na Rais wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

 

Nyota huyo kunako tuzo hizo aliwabwaga chini wakongwe na nyota kama Mbwana Samatta, Nadir Haroub Cannavaro pamoja na Sophia Mwasikili, ambapo, mbali na tuzo hiyo pia alichukua nyingine mbili ambazo ni Mwanamichezo Chipukizi akimbwaga chini Aishi Manula wa Azam FC pamoja na Mwanasoka bora wa kike akimpiga chini Sophia Mwasikili.

Kaijage ametangaza program yake ya  mazoezi itakayochukua takribani wiki nne (4) ili kuhakikisha wachezaji wanakua tayari kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kati ya Machi 21, 22 mwaka huu, huku akipanga kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuelekea Lusaka Zambia kwenye mchezo wa awali.

 

Twiga Stars ambayo itakua kambini katika Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF zilizopo Karume,  imeingia moja kwa moja katika hatua ya pili kucheza na Zambia kufuatia kuwa na matokeo mazuri katika msimamo wa viwango vya soka la wanawake barani Afrika.

 

Wachezaji wengine ambao wameitwa kikosini ni, Asha Rashid, Esther Chaburuma, Fatuma Bushiri, Fatuma Hassan, Fatuma Mustapha, Fatuma Omari, Eto Mlenzi, Mwajuma Abdallah, Sofia mwasikili, Zena Khamis, Mwanahamis Omar, Fatuma Khatibu, Fadhira Hamad, Anastazia Anthony.

 

Pamoja na Thereza Yonna, Happines Hezron, Amina Ally, Donizia Daniel, Fatuma Issa, Vumilia Maarifa, Maimuna Hamisi, Najiati Abbasi, Stumai Abdallah, Ziada Ramadhani, Zuwena Aziz, Irene Joseph (Mfunzo – Zanzibar), Dawa Haji Vuai (JKU – Zanzibar), Belina Julius na Amina Ramadhani.



Comments