Alichosema Omog baada ya kugawana pointi na Prisons



Alichosema Omog baada ya kugawana pointi na Prisons

joseph-omong-kocha-wa-Azam-fcNa. Richard Bakana, Dar es salaam

Kocha mkuu wa Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania bara , Azam FC, Mcameroon, Joseph Omog, amekili kuwa mtanange wa jana dhidi ya Tanzania Prisons ulikiwa mgumu sana kwake licha ya kuwa katika maandalizi ya klabu Bingwa.

Akiongea na Shaffihdauda.com baada ya mchezo huo kumalizika kwa kugawana pointi moja moja (0-0), kocha huyo ambaye ameweka rekodi ya kuwa wa kwanza kuipatia Azam FC kikombe cha kwanza cha VPL, amesema kwasasa anahamishia mawazo katika mchezo wa klabu bingwa kama kweli wanataka kusonga mbele.

"Mchezo ulikuwa mgumu sana kwetu, Prisons ni timu nzuri sana lakini nashukuru tumetoa sare, Tumepata sare mbili mfululizo, sasa tunataka kuwa makini na mchezo wa Jumamosi kama tunataka kusonga mbele klabu bingwa" Amesema Omog ambaye wiki hii anakibarua kizito dhidi ya Al Merreikh huko Sudan ambako atakuwa akisaka ushindi au sare ili aweze kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika.

Kwa upande wake Kocha wa Tanzania Prisons, David Mwamaja yeye ameanza kwa kuwasifia wachezaji wake kwa matokeo aliyoyapata licha ya kusema kuwa hajaridhishwa maana alitaka kuibuka na pointi tatu.

"Vijana wangu wamejitahidi kufanya vizuri lakini sio vizuri zaidi, maana kufanya vizuri tungepata ushindi lakini nawapongeza kwasababu wenzetu wamejiandaa vizuri zaidi" Amesema Kocha wa Prisons, David Mwamaja baada ya mchezo huo uliopigwa kunako uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam na kumalizika usiku wa jana.

Kwa matokeo hayo sasa Azam FC inakuwa inazidi kuachwa mbali na wapinzani wao Yanga SC ambao kwa sasa wanashikilia usikani wa Ligi wakiwa na pointi 41, huku mabingwa hao watetezi wakiwa na pointi 27, baada ya kucheza michezo 15, kufunga 7, sare 6 kufungwa 2.



Comments