Nahodha wa Manchester City Vincent Kompany amesisitiza kuwa kipigo cha kuduwaza walichokipata kutoka kwa Arsenal, hakitawavunja nguvu na haitakuwa mwanzo wa wao kupunguza ari ya kutetea taji lao.
City ilifungwa na Arsenal 2-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani Etihad Stadium na kufanya wawe nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku zikiwa zimesalia mechi 26.
Wapigania taji hao wawili (City na Chelsea) wanakutana Stamford Bridge Januari 31, mchezo ambao bosi wa Manchester City Manuel Pellegrini amekiri kuwa kama kweli wanataka kutetea taji, basi hawastahili kuupoteza mchezo huo.
Lakini nahodha wa City Vincent Kompany amedai kufungwa na Arsenal kunamaanisha kuwa ndiyo kwanza moto unakolea na kwamba hasira zao zote sasa zinaelekezwa kwenye mechi ya Chelsea.
"Kinadharia, hali sasa itakuwa bora zaidi kwetu kwasababu tutaongeza ari, huo ndio ukweli wenyewe," alisema Kompany. "Siku zote huwa tunakuwa bora kwenye michezo kama hii, tunajipanga."
Comments
Post a Comment