VAN PERSIE ASEMA HAJUI KAMA ATASAINI MKATABA MPYA MANCHESTER UNITED …akiri kuwa kiwango chake kimeporomoka
Robin van Persie amekiri kuwa soka lake msimu huu halipo kwenye kiwango bora na hajui kama Manchester United watampa mkataba mwingine pindi huu wa sasa utakapofika ukingoni miezi 18 ijayo.
Van Perise ambaye aliipa United taji la Premier League kufuatia magoli 26 aliyofunga katika msimu wake wa kwanza mwaka 2012 akitokea Arsenal kwa pauni milioni 24, amesema atajitahidi kadri ya uwezo wake kufufua kiwango chake.
Anasema amekuwa akijiuliza mwenyewe kuhusu mchango wake kwa timu msimu huu na kubaini kuwa ana deni kubwa.
"Msimu huu nimecheza mechi kama 20 hivi na kufunga magoli nane – sina raha na hilo. Nahitaji kufunga zaidi," alisema Van Persie.
"Nitafanya kila niwezalo, kila siku si mazoezini si kwenye mechi, nitafanya yale ambayo nimekuwa nikifanya katika miaka 10 iliyopita ambapo magoli yalikuwa yakimiminika nyavuni."
Van Persie atatimiza miaka 32 mwezi Agust na atakuwa nje ya mkataba wake Old Trafford kiangazi cha mwaka 2016. United bado haijaanzisha maongezi ya mkataba mpya na mshambuliaji huyo wa Uholanzi amesema jambo hilo liko nje ya uwezo wake.
"Ni nje ya uwezo wangu, kwa sasa nachoweza kusema ni kwamba nitakuwa hapa kwa miezi 18. Uhuo ndio ukweli. Siwezi kuangalia hatma yangu, sijui nini kitatokea baada ya hapo. Tunapaswa kusubiri na kuona nini kitatokea."
Comments
Post a Comment