TORRES APELEKA KILIO BERNEBE, REAL MADRID YATEMESHWA NA ATLETICO MADRID TAJI LA KWANZA …sasa Atletico kukutana na Barcelona nusu fainali
Fernando Torres anafungua ukurusa mpya katika historia yake baada ya kufunga bao lake la kwanza ndani Santiago Bernabeu, kitu ambacho hakawahi kufanya hapo kabla akiwa na timu yoyote ile.
Hiyo ilikuwa katika mechi kali marudiano ya kombe la Copa del Rey kati ya Atletico Madrid na Real Madrid iliyokuwa uwanja wa nyumbani ikipambana kufuta bao 2-0 ilizofungwa na Atletico kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita.
Torres akatupia bao mbili na kuisadia Atletico Madrid kulazimisha sare ya 2-2 na kusonga mbele kwa jumla ya bao 4-2, hii ikimaanisha kuwa Real Madrid wametema taji la kwanza miongoni mwa mataji manne waliyoshinda mwaka jana.
Hii ni awamu ya pili kwa Torres kuichezea Atletico Madrid timu yake ya tangu utotoni kabla hajaenda Liverpool, Chelsea na AC Milan.
Katika awamu yake ya kwanza ya kuitumikia Atletico, Torres hakuwahi kuifunga Real Madrid hata bao moja, jambo lilifanya mashabiki waliofurika Santiago Bernabeu Alhamisi usiku wamkejeli wakiamini kuwa hana madhara yoyote kwao.
Lakini ilimchukua Torres sekunde 49 tu kuwajibu mashabiki hao baada ya kuifungia Atletico bao la kwanza lililowafanya Real Madrid wawe na mlima mrefu wa kupanda.
Beki Sergio Ramos akasawazisha kwa kichwa dakika ya 20, kabla ya Torres ambaye alifunga bao moja tu katika miezi yake minne aliyoichezea AC Milan, hajaifungia Atletico goli la pili dakika ya kwanza tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Mchezaji bora wa dunia Cristiano Ronaldo akaifungia Real Madrid bao la pili dakika ya 54. Safari ya Real Madrid kutetea kombe hilo la Mfalme ikakomea hapo.
Kwa matokeo hayo, Atletico sasa itakutana na Barcelona katika hatua ya nusu fainali.
Comments
Post a Comment