TAMASHA LA CDS LILIVYOFANA DAR ES SALAAM …bendi zafunikana, sasa kufanyika kila mwaka, wasanii wa nje kualikwa
Tamasha kubwa la muziki wa dansi lililofanyika TCC Club Chang'ombe Jumapili usiku, lilifana sana huku kila bendi ikionyesha ufundi wake.
Mamia ya watu waliojazana uwanjani hapo wakashuhudia bendi nne za dansi zikichuana vikali kwa kusindikizwa na kundi la taarab la Ogopa Kopa chini ya malkia Khadija Kopa.
Mapacha Watatu walifungua pazia la burudani za tamasha hilo wakafuatiwa na Msondo, FM Academia, Ogopa Kopa kabla Malaika Band chini ya Christian Bella hawajafunga pazia.
Hata hivyo kabla ya Mapacha Watatu, kulikuwa na burudani za kupasha moto kutoka kwa bendi ya walemavu – Tunaweza Band pamoja na ngoma za asili.
Tamasha hilo lilirindima kuanzia saa 12 za jioni hadi saa 9 za usiku. Maandalizi yalikuwa ni mazuri sana na hakuna hata mtu mmoja aliyekosa kiti, lakini pia hakukuwa na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Aliyekuwa MC wa tamasha hilo Khamis Dacota, akasema kuwa CDS (Kampuni ya kusafirisha vifurushi) chini ya mkurugenzi wake Masoud Wannani, imeamua kulifanya tamasha hilo liwe la kila mwaka na kuanzia mwaka ujao, litakuwa likisindikizwa na msanii nyota wa muziki wa muziki wa rumba kutoka nje ya nchi.
Kama kweli tamasha hili litakuwa likifanyika kila mwaka basi utakuwa ni ukombozi mkubwa wa muziki wa dansi ambao umekuwa ukitengwa kwenye matamasha makubwa ya muziki.
Kiushindani, bendi zote zilizotumbuiza zilipiga mzigo wa maana japokuwa ni bendi mbili za dansi ndizo zilizofunika zaidi. Kwa manufaa ya tamasha la mwakani tunadhani si sahihi kuzitaja bendi hizo .Huu si wakati wa kuvunjana moyo, ni wakati wa kuwapongeza waandaji na washiriki wote kwa KUTHUBUTU. Pata picha kadhaa.
Comments
Post a Comment