STARS MABORESHO YATAMBA KUFANYA KWELI KWA WANYARWANDA KESHO


STARS MABORESHO YATAMBA KUFANYA KWELI KWA WANYARWANDA KESHO

IMG_8768

Na Bertha Lumala
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij ametamba kuwa kikosi cha Taifa Stars Maboresho kitakachokivaa kikosi cha taifa ya Rwanda (Amavubi), kitashinda mchezo wa kesho utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye hoteli ambayo Taifa Stars Mabaresho imefikia jijini Mwanza, Nooij amesema kikosi hicho kinachoundwa na wachezaji wa umri wa chini ya miaka 22, kimejiandaa vya kutosha kukabiliana na wapinzani wao hao katika mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa.

"Ni kikosi kinachoundwa na wachezaji wengi vijana wanaofanyiwa maandalizi ya kucheza mashindano ya kimataifa ya CHAN hapo baadaye, tumejipanga vizuri katika mechi hii ya kujipima nguvu," amesema Nooij.

Amesema timu hiyo ya maboresho licha ya michezo yake miwili kufanya vibaya dhidi ya timu ya taifa ya Burundi, anaamini itafanya kweli kesho kutokana na wachezaji mahiri walioitwa wakiwamo Simon Msuva (Yanga) na Said Khamis Ndemla (Simba).

Awali kocha msaidizi wa timu hiyo, Salum Mayanga, ametangaza majina ya wachezaji 22 kati ya 26 wa Stars Maboresho ambao iwapo watakubaliana na Amavubi itakayoongozwa na Haruna Niyonzima anayechezea Yanga ya jijini Dar es Salaam, watavalishwa jezi wote.

Mayanga amewataja wachezaji wa Stars ni Manyika Peter, Benedictor Tinoco, Miraji Adam, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Edward Charles, Salum Telela, Hassan Banda, Said Juma na Ndemla Said.

Wengine ni Abubakar Ally, Hassan Dilunga, Shiza Ramadhani, Simon Msuva, Salum Mbonde, Rashid Mandawa, Alfred Juma, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Kelvin Friday, Adam Paul, Hussein Moshi na Joram Mgeveke.

Mayanga amesema wachezaji Aishi Manula (Azam), Emmanuel Semwanda (Africana Lyon) na Green Atupele (Kagera Sugar), wameondolewa kutokana na kucheza mechi za ligi juzi, huku Omary Nyenje wa Ndanda akisumbuliwa na goti.

Manahodha wa Stars, Msuva na Ndemla wote wameungana na kocha wao kuipa nafasi timu hiyo kushinda dhidi ya Amavubi kesho.



Comments