PICHA 20: OGOPA KOPA WALIVYONGURUMA ‘NYUMBANI LOUNGE’ IJUMAA USIKU …Khadija Kopa moto chini, Young Hassan Ali usipime
Kundi jipya la miondoko ya taarab, Ogopa Kopa Classic Band, Ijumaa usiku lilijipima ubavu kwa onyesho lao la kwanza jijini Dar es Salaam ndani ya ukumbi wa M.O.G zamani Nyumbani Lounge.
Kitu kimoja kilikuwa wazi katika onyesho hilo – Ogopa Kopa wametumwa kuja kufanya kazi, walipiga show ya kutakata.
Licha ya kwamba mahudhurio hayakunona sana, lakini kilichoonekana jukwaani ni utumbuizaji mzuri kupitiliza.
Kila msanii aliyesimama jukwaani kuimba alikuwa na mvuto wake, kila mmoja alikuwa na utofauti wake.
Wapiga vyombo Jumanne Ulaya (solo), Shomar Zizzou na Hamad (Bass) Said Mabomba na Omar Zungu (kinanda) walikuwa wameshikana vizuri sana.
Mwimbaji Anifa Maulid "Jike la Chui" ambaye pia ndiye aliyekuwa MC, alifanya vizuri na wimbo wake mpya "Stop Red Card", Shadya Shombeshombe akatesa na "Aanzae Havumi" huku Black Kopa akitakata na kitu "Full Ku-enjoy".
Young Hassan Ali kupitia wimbo wake "Chozi la Mnyonge" akathibitisha kuwa ni mkali wa kutawala jukwaa.
Mwimbaji huyo ambaye pia ni mkurugenzi wa muziki (Director), alijua kucheza na sauti yake, akajua namna ya kuchezesha watu kwenye ngoma chini, lakini pia alivutia kwa unadhifu wake, alipendeza sana.
Malkia Khadija Kopa, nani asiyeujua uwezo wake? Hakuna. Aliiteka show, popote alipokaa angeliteka jicho lako – kuanzia alipokuwa kwenye safu ya waitikiaji hadi aliposimama kuimba.
Kupitia nyimbo za "Mjini Chuo Kikuu" na "Mamaa Mukubwa" Kopa alisisimua kwa kila jambo – uimbaji, uchangamfu, kujiamini pamoja na nyonga za kufa mtu.
Mandhari ya ukumbi ilikuwa ni bab kubwa, unakula muziki wa nguvu huku unapulizwa na kiyoyozi (AC), ustaarabu ndiyo usiseme, ni sehemu ya 'kishua' usalama asilimia 200.
Comments
Post a Comment