Mashabiki Yanga waingilia vita ya Amissi Tambwe na Mliberia


Mashabiki Yanga waingilia vita ya Amissi Tambwe na Mliberia
KATIKA hali isiyotarajiwa, mashabiki wa Yanga waliokuwa na dukuduku la moyoni, juzi Alhamisi jioni walimfuata Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Boniface Mkwasa na kumtaka abadilishe mpangilio ili badala ya kumtumia straika Mrundi, Amissi Tambwe kuwa straika wa pili, amchezeshe akiwa  straika namba moja na Mliberia, Kpah Sherman, ndiye awe straika namba mbili.

"Samahani kocha kwanza pole na kazi, tulikuwa na maoni kwamba Tambwe acheze namba  tisa na Sherman acheze 10, maana tuliona katika Kombe la Mapinduzi mlikuwa mnawabadilisha sasa tumeona Tambwe anamudu sana tisa hapo tutapata mabao mengi," alisema mmoja wa mashabiki hao huku akiungwa mkono na wenzake waliomzunguka Mkwassa kwenye Uwanja wa Boko Vetereni.

Katika kutoa ufafanuzi,  Mkwasa aliwaambia kuwa hivyo ndivyo walivyopanga kuwachezesha kwa kuwabadilisha ili kuwazoesha wasikariri namba moja.

Jibu hili lilionekana kutowaridhisha mashabiki hao, lakini  walimshukuru kocha huyo na kisha kumwambia tangu wameanza kukinoa kikosi hicho kimekuwa na mabadiliko makubwa na kinawapa matumaini ya kufanya vema katika mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

Katika hatua nyingine, beki wa Yanga ambaye pia ni nahodha, Nadir Haroub 'Cannavaro' amemwambia kocha wa Simba, Goran Kapunovic, kuwa  kazi si kuchukua Kombe la Mapinduzi, bali kushinda mechi za Ligi Kuu Bara.

"Tunaamini Yanga nzuri ingawa tulitolewa katika Kombe la Mapinduzi, mechi zile si kipimo kwamba timu yake ni nzuri. Huku kwenye ligi ndiyo sehemu ambayo Simba inatakiwa kuonyesha ubora wake,"alisema Cannavaro.

"Nimeona watu wanampongeza sana huyu kocha mpya wa Simba hata mimi nampongeza kwa ubingwa wa Mapinduzi, lakini  ili watu wajue ubora wake anatakiwa ashinde mechi za ligi."

Comments