MANENO UVURUGE MPIGA GITAA MAHIRI, UNAJUA ALITOKA WAPI?



MANENO UVURUGE MPIGA GITAA MAHIRI, UNAJUA ALITOKA WAPI?
10427257_673306419451675_4241579221547754953_n

MANENO UVURUGE

Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake ambao n marehemu Jumanne na Stamili, ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania. Kaka yake mwingine Huluka, ni mpiga gitaa mahiri aliyeko katika bendi ya Msondo Group. Jumanne Uvuruge ndie aliyekuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, na ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu, kuna maelezo kuwa wimbo ule ulitokana na hadithi ya ukweli iliyomtokea mtunzi. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na kisha kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.

Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa. Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa alilotengeneza kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza, jambo la kawaida sana wakati wa kujifunza kupiga magitaa. Jumanne na Stamili waliamua kuanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Generation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga magitaa ya rythm enzi hizo. Katika kupiga huku na huko na rafiki zake hatimae akakutana na Freddy Benjamin Hinju, mwanamuziki muimbaji ambaye sasa ni marehemu na huyu ndie aliyemshauri kujiunga na Bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia. Lakini Maneno alipofika UDA pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa Katibu wa bendi hiyo, ikalazimika aachane na UDA. Freddy alimuombea kazi Super Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B, na hapo akakutana na wanamuziki kama Mzee Hatibu Iteytey aliyekuwa mpiga sax, Nuzi Ndoli, Rocky, Mzee Bebe, wakati huo akina Eddy Sheggy walikuwa bado hawajajiunga na bendi hii.
Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya uimbaji wao kwenye ule wimbo Milima Ya Kwetu, marehemu Banza Tax nae alijiunga na bendi hiyo kipindi hiki.

Bendi iliyokuwa na makao makuu kule Mabibo, katika bar iliyokuwa inaitwa Lango la Chuma, bendi ya Tchimanga Assossa Orchestra Mambo Bado, ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa muimbaji na Nana Njige pia wakajiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Orchestra Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliiacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waliingia Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa wa kupiga gitaa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa.

uvuruge 1

Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo

Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Orchestra Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba. MMoja ya wanamuziki wa Maquis Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma, iliyokuwa imedorora, Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma. Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo mpiga sax, na Mzee Mponda mpiga gitaa mahiri ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo Msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Villa Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa.
 

 



Comments