KUZALIWA KWA MLIMANI PARK ORCHESTRA………………..



KUZALIWA KWA MLIMANI PARK ORCHESTRA………………..

mlimani02NILIPATA bahati ya kuongea na mmoja wa wanamuziki wakongwe waliowahi kupitia bendi ya Mlimani Park Orchestra, na kumuuliza sababu za bendi ya Mlimani Park Orchestra kuzaliwa ikiwa imeundwa na kundi kubwa la wanamuziki kutoka Dar International Orchestra. Haya ndio maelezo yake. "Kutokea kwa bendi ya Mlimani kuanza na kundi kubwa la Dar International ilikuwa ni kwa bahati sana"

Kwa maelezo yake mwanamuziki huyu aliyekuwepo wakati huo, hadithi nzima ilitokana na bendi ya Dar International kukodishwa na wanafunzi wa Chuo Cha Ardhi katika sherehe yao ya kuwaaga wanachuo wa zamani na kukaribisha wapya. Chuo cha Ardhi kilikodi ukumbi wa Mlimani Park kwa ajili ya shughuli hiyo. Wakati huohuo utawala wa Mlimani Park ulikuwa mbioni kutengeneza bendi baada ya kumalizika mkataba wa Orchestra Fukafuka katika ukumbi huo. Tchimanga Assossa ambaye alikuwa amekuja na Bendi ya Fukafuka alibaki nchini na alikuwa katika hatua za mwisho za mazungumzo na uongozi huo ili kwenda kufuata wanamuziki wengine kutoka Kongo kwa ajili ya bendi ya ukumbi huo. Hivyo basi Dar International Orchestra, wakati huo ndio wakivuma na nyimbo kama Magreti walianza kuporomosha muziki chini ya kiongozi wao Abel Balthazal. Uongozi wa Mlimani Park ulipigwa butwaa na muziki wa hawa jamaa, Abel aliitwa pembeni na kuulizwa bendi iko chini ya mkataba wa nani? Na je, wanamuziki wangeweza kukubali kuajiriwa na na Mlimani Park wakati huo ikiendeshwa na TTTS? Kwa vile Dar International ilikuwa ya mtu binafsi na hawakuwa na ajira yoyote ya kudumu katika bendi hiyo, haraka sana wanamuziki walikubali wazo hilo la kuwa na mikataba maalumu na hivyo kuwa na uhakika wa ajira. Siku hiyo Abel aliwaambia wanamuziki wenzie kujitahidi katika kila nyanja, kupiga vizuri kuwa na nidhamu ya hali ya juu, kuwezesha uongozi huo kuhamasika kuwapa mikataba hiyo. Kesho yake viongozi wa Dar International walienda kukutana na viongozi wa ukumbi wa Mlimani Park, na wakakubaliana kuazisha kambi ya bendi mpya palepale katika ukumbi wa Mlimani. Haikuwa taabu maana vyombo vilivyonunuliwa wakati wa mkataba wa Orchestra Fukafuka vilikuwa mali ya Mlimani Park. Abel Barthazar na viongozi wenziwe walisisitiza kuwapata wanamuziki kama Muhidin Gurumo, inafaa hapa ikumbukwe kuwa ni huyuhuyu Abel ndiye aliyeisuka Dar International Orchestra baada ya kuwachukua wanamuziki wote wa Safari Trippers wakati huo, akiwemo Kassim mponda, Joseph Bernard, Marijan Rajabu, Ben Peti, Zito Mbunda,Bito Elias na wengine akamuacha Christian Kazinduki na kutoka Tanzania Stars ya Maggot walitoka Joseph Mulenga, George Kessy , Haruna Lwali na wengineo, na kwa staili hiyohiyo skwadi nzima ya Dar International Orchestra ikageuka kuwa Mlimani Park Orchestra.

Muda mfupi kabla ya tukio hili la kihistoria, ugomvi mkubwa ulikuwa umetokea Dar International kati ya Marijani Rajabu na Abel Balthazar, katika ubishi kuhusu tungo aliyoleta Marijani ambayo Balthazar alidai kuwa ni ya Tabu Ley kwa hiyo akatunge tena, jambo lililoleta kushikana mashati, na kusababisha Marijani kusimamishwa kazi. Wakati yuko benchi ndipo mpango mzima wa kuhamia Mlimani ulifanyika hivyo mwenye vyombo alilazimika kumfwata tena Marijani na kumwomba aunde bendi upya, na ndipo Super Bomboka ikaundwa. Mlimani Park ikaanza ikiwa na Tchimanga Assossa ambaye safari ya kwenda kutafuta wanamuziki Kongo ikawa imekufa. Na mchango wa kudumu wa Assossa wakati huo ni utunzi wa ule wimbo Gama. Assossa aliondoka hatimae na kujiunga na Orchestra Makassy

 

 



Comments