Winga wa Real Madrid Gareth Bale amefutilia mbali uwezekano wa yeye kujiunga na klabu ya Manchester United kwa kusema haoni nafasi yake klabuni hapo na kwamba ana furaha kuendelea kuitumika timu yake ya sasa ya Real Madrid.
Kumekuwa na tetesi kuwa nyota huyo atajiunga na Manchester united huku kipa David De Gea akielekea Real Madrid kama sehemu ya mpango huo. "Siioni nafasi yangu katika timu hiyo, nafurahi kushinda mataji. Nataka kuendelea kufanya hivi nikiwa na Real Madrid."
Bale alijiunga na Real Madrid kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 85 iliyovunja rekodi ya usajili duniniani mwezi septemba 2013.
Mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham alilaumiwa na baadhi ya mashabiki wa Madrid kwa kumnyima pasi Cristiano Ronaldo kwenye michezo dhidi ya Espanyol.
Bale anasema "Napata sapoti nikiwa hapa Bernabeu. Nitaendelea kuonyesha nini naweza kufanya uwanjani na kuendelea kutwaa makombe". Sidhani kama nina tamaa uwanjani ninasaidia kufunga magoli na kufunga, ninacheza vile ninavyotakiwa kucheza, acha vyombo vya habari viseme watakavyo".
Akizungumzia uhusiano wake na Ronaldo nyota huyo wa kimataifa wa Wales, aliongeza "hakuna uadui kati yetu."
Bale amefunga mabao 36 na kusaidia kutoa pasi za mabao 26 katika michezo 72 aliyoichezea Real Madrid.
Comments
Post a Comment