YANGA SC: TUTASHIRIKI MAPINDUZI CUP MWAKANI



Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, wamethibitisha watapeleka kikosi chao Visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi mwakani.

Timu nne kutoka Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Azam FC, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zimealikwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika Zanzibar kuanzia Januari 1-13 mwakani.
kp
Katibu Mkuu mpya wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, amethibitisha ushiriki wa kikosi chao katika mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya tisa tangu yaanzishwe.

"Yanga itashiriki Kombe la Mapinduzi mwakani. Tumeshauandikia barua uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ili wapangue ratiba ya mechi yetu ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union iliyopangwa kuchezwa Januari 10 jijini Tanga," amesema Tiboroha.

Mbali na Yanga, tayari kocha mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri na kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime wameshathibitisha ushiriki wa timu zao katika michuano hiyo huku timu ya AFC Leopards ya Kenya ikijitoa baada ya kupewa mwaliko.

Timu 12 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo mwakani kama ilivyothibitishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibra (ZFA), Kassim Haji Salum. Mbali na klabu nne za VPL na AFC Leopards waliojitoa, mabingwa watetezi KCCA ya Uganda pia wamealikwa.

Timu nyingine zilizoalikwa ni pamoja na mabingwa wa Zanzibar KMKM, Polisi FC, JKU, Mtende Rangers na Shaba FC.

Ikiwa chini ya Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic, Simba ilifungwa bao 1-0 dhidi ya KCCA katika mechi ya fainali mwaka huu huku Yanga 'wakijipiga faini ya Sh. milioni 10′ kwa kuipatia kamati ya mashindano hayo baada ya kutoshiriki kwa miaka miwili mfululizo.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameshaweka wazio kwamba wameshapokea barua ya ZFA kuhusu ushiriki wa timu nne za Tanzania Bara katika michuano hiyo mwakani lakini wanaishughulikia kabla ya kutoa taarifa rasmi.



Comments