Akihutubia mamia ya mashabiki wa soka waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Mwanakalenge uliopo Bagamoyo, Pwani kushuhudia fainali ya Kombe la Kawambwa jana, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa alisema uongozi mpya wa TFF umeweka nguvu nyingi katika soka la vijana kuhakikisha vipaji havipotei bure.
"(Shukuru) Kawambwa ametonesha vipaji vya soka vilivyopo kwenye jimbo lake. Kama mnavyojua uongozi mpya a TFF chini ya Rais Jamal Malinzi umeweka nguvu nyingi katika kuinua soka la vijana.
"Sehemu kubwa ya wachezaji katika michuano hii tumeona ni vijana ambao wanahitaji kuendelezwa ili vipaji vyao visipotee bure," alisema kiongozi huyo aliyekuwa mgeni rasmi.
Aidha, Mwesigwa ambaye alikuwa amemwakilisha Rais wa TFF, Malinzi, alitoa zawadi ya mipira sita kwa timu nne zilizotinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mwaka huu ambao Timu ya Zing Zong imenyakua ubingwa baada ya kuifumua mabao 2-1 Timu ya New Star.
Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa michuano hiyo katika ustawi wa soka na jamii, TFF imeamua kutoa mipira hiyo yenye hadhi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
TFF kupitia kwa Mwesigwa ilitoa mipira minne
kwa timu zilizoshika nafasi ya tatu na nne huku mshindi wa kwanza na wa pili wakipatiwa mipira miwili pamoja na seti mbili za jezi, kila timu ikipata seti moja.
"TFF inawapongeza sana kwa kuonesha uwezo mkubwa na kucheza kwa kujituma mpaka mmefika hatua hii," alisema.
Mbali na kuipongeza TFF kwa juhusi ilizonazo katika kuendeleza mpira wa Tanzania, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kawamba, ambaye ndiye mdhamini wa mashindano hayo, alitoa zawadi ya pikipiki nane kwa washindi wa kila kata za jimbo lake na bingwa a nmichuano hiyo, Timu ya Zing Zong.
Kiongozi huyo wa serikali pia alitoa zawadi za kombe kwa mchezaji bora, kipa bora, mwamuzi bora na mfungaji bora wa michuano hiyo wakijipatia kombe huku akitoa zawadi za fedha kwa washindi wa michezo ya kufukuza kuku.
Comments
Post a Comment