SERIKALI ZANZIBAR YAINGILIA KATI KUNUSURU KOMBE LA MAPINDUZI


SERIKALI ZANZIBAR YAINGILIA KATI KUNUSURU KOMBE LA MAPINDUZI

Kombe la Mapinduzi

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Wakati klabu zote za Kenya zimejitoa kushiriki Kombe la Mapinduzi mwakani, michuano hiyo iko shakani kufanyika kutokana na baadhi ya wadau wa soka Visiwani Zanzibar kukimbilia mahakamani.

Hata hivyo, imeelezwa leo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelazimika kuingilia kati mgogoro unaoendelea miongoni mwa viongozi wa ZFA na kuiondoa kesi mahakamani ili kuyanusuru mashindano hayo.
 
Klabu mbili za Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Tusker FC na AFC Leopards zilizokuwa zimealikwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), zimejitoa huku Yanga wakithibitisha 'kienyeji' (bila barua) ushiriki wao katika mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika kuanzia Januari 1-13 mwakani.

Licha ya Katibu Mkuu mpya wa Yanga, Jonas Tiboroha kuvithibitishia vyombo vya habari wiki iliyopita kushusu kujitosa kwao kushiriki Kombe la Mapinduzi mwakani, taarifa ambazo zimepatikana kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimeeleza kuwa ni klabu moja tu kati ya Tanzania Bara iliyothibitisha rasmi kushiriki katika mashindano hayo.

Timu nne za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga ni miongoni mwa timu 12 zilizoalikwa kushiriki michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya tisa tangu ianzishwe kuenzi Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

"Mpaka sasa ni Simba tu waliothibitisha rasmi kushiriki Kombe la Mapinduzi. Hata Simba nao wamesema wanapeleka kikosi cha pili, kinyume cha kanuni za mashindano hayo," chanzo chetu ndani ya TFF kimeeleza.

"TFF yenyewe haijajibu barua ya ZFA kutokana na kesi iliyopo mahakamani huko Zanzibar, lakini lolote linaweza kufanyika kwa sababu michuano ya Kombe la Mapinduzi ni ya kisiasa, linaweza kutoka agizo kutoka kwa wakubwa serikalini," kimesema zaidi chanzo chetu.

Desemba 17, mwaka huu Mahakama Kuu ya Zanzibar kupitia Jaji Mkusa Isack ilitoa oda ya kuwasimamisha Rais, Makamu wa Rais na Katibu Mkuu wa ZFA (Pemba) kujishugulisha na kazi yoyote inayohusu chama hicho pamoja na kusimamisha mchakato wa Katiba na kufunga akaunti ya chama hicho isiingize wala kutoa fedha.

Kesi hiyo inadaiwa kufunguliwa Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Alhaji Haji Ameir akishirikiana na Mwenyekiti wa ZFA wilaya ya Chakechake, Ali Bakari.

Klabu nyingine zilizoalikwa kushiriki michuano hiyo mwakani ni pamoja na mabingwa watetezi KCC FC ya Uganda, mabingwa wa Zanzibar, KMKM, Shaba FC, Polisi FC na JKU, Mtende Rangers, zote za Ligi Kuu ya Zanzibar.

Ratiba ya Kombe la Mapinduzi hadi sasa haijatoka huku KCC FC, mabingwa watetezi wakijiandaa kutoka Uganda kwenda Zenj tayari kwa michuano hiyo.



Comments